Wanawake waliobakwa nchini Sudan, hufa kwa kujiua, wanaharakati wanasema,
Wanawake waliobakwa nchini Sudan, hufa kwa kujiua, wanaharakati wanasema,
Habari hii ina maelezo ambayo baadhi yanaweza kuhuzunisha.
Wanawake kadhaa wamejitoa uhai katika jimbo la kati la Gezira nchini Sudan baada ya kubakwa na wapiganaji wa kijeshi katika vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini humo, makundi ya kutetea haki za binadamu na wanaharakati wamesema.
Ripoti hizo zinakuja baada ya wanamgambo wa RSF kushutumiwa na Umoja wa Mataifa kwa "uhalifu wa kikatili", ikiwa ni pamoja na mauaji ya halaiki, katika jimbo hilo wiki iliyopita.
Huku wapiganaji wa RSF wakiendelea kusonga mbele, shirika moja la kutetea haki za binadamu limeiambia BBC kuwa linawasiliana na wanawake sita ambao wanafikiria kujiua huku wakihofia kudhulumiwa kingono.
Lakini RSF imetupilia mbali ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inayolaumu kuongezeka kwa unyanyasaji wa kingono kwa wapiganaji wake, ikiiambia BBC kwamba shutuma hizo "hazikuwa na ushahidi".
Mapambano makali ya kugombea madaraka kati ya wanamgambo wa RSF yamesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kuwalazimisha zaidi ya watu milioni 11 kuondoka makwao tangu mzozo huo uanze Aprili 2023.
Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, Cindy McCain, alitembelea kituo cha misaada cha Port Sudan wiki hii, na aliambia BBC kuwa nchi hiyo inaweza kukumbwa mzozo mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kutokea duniani ikiwa usitishaji mapigano hautafikiwa.
Alionya kuwa mamilioni ya watu wanaweza kufa kutokana na njaa.