Waridi wa BBC: Namna ujauzito ulivyonisababishia usikivu hafifu
Waridi wa BBC: Namna ujauzito ulivyonisababishia usikivu hafifu

Chanzo cha picha, Rukia Jamal
”Huyu hata ukimpigia simu hatapokea anakwambia tuma ujumbe, masikio yake mazito,” anaeleza Rukia Jamal ambaye ana changamoto ya usikivu hafifu akinukuu baadhi ya maneno ya wateja wake.
Rukia, mwenye umri wa miaka 26 ni mama wa mtoto mmoja wa kike mwenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijami amekuwa akikabiliana na unyanyasaji kutokana na ulemavu alio nao.
Kwa baadhi ya watu katika jamii suala la ulemavu ni tiketi ya kujitumbukiza katika utegemezi wa misaada na wengine hata kuwa ombaomba.
Rukia anaelezea kuwa wanajamii wana uelewa duni juu ya watu wenye usikifu hafifu. ”Zipo nyakati ambazo nilichapisha tangazo la biashara zangu mtandaoni baadhi ya watu waliandika kunikejeli kuwa masikio mazito kwa kuwa niliwahimiza kuandika ujumbe badala ya kuzungumza.”
Anaongeza kuwa baadhi ya watu katika jamii humuona mwenye tatizo kubwa, lakini kwake hilo halijamzuia kumudu shughuli zake zote zinazohusu kujitafutia kipato.
Maisha kwenye mitandao ya kijamii

Chanzo cha picha, Rukia Jamal
Rukia alieleza BBC kuhusu visa na mikasa ambavyo hukumbana navyo katika kujitafutia riziki kwa kuuza bidhaa zake mitandaoni.
‘’Zipo nyakati nilizopoteza wateja kutokana na baadhi yao kupenda kupiga simu tu, ninapowaambia tumia ujumbe wa maandishi kuwasiliana, bila kupokea simu huondoka na kunisema kwenye ukurasa wangu kwamba mimi ni muongo na tapeli,’’ alisema na kuongeza; ”Hali hii hunifanya nijiskie vibaya sana lakini kwa vile kuna watu wana matatizo makubwa kuliko yangu, mfano wasio na mikono au miguu basi hunibidi niichukulie tu kama kitu cha kawaida.”
Aacha mtoto kutafuta riziki
Rukia anasema wakati anaanza shughuli za biashara, mnamo Desemba 2018 alimuacha mwanaye kwa mama yake mzazi akiwa na miezi 11, ili akapambane kutafuta riziki visiwani Zanzibar.
Anaeleza kuwa ni baada ya kupokea simu kutoka kwa kampuni moja huko Zanzibar ikimuhitaji kwenda kuanza ajira kama katibu mukhtasi (secretary).
Rukia ambaye alihitimu masomo ya stashahada ya utunzaji wa kumbukumbu mwaka 2016 anasema, ”Nilipofika huko (Zanzibar) nilikabidhiwa shughuli ya kutembeza bidhaa majumbani kama vyombo, lakini nikamweleza meneja kuwa hiyo si kazi mliyoniitia, alikataa na kwa kuwa sikuwa na nauli ya kurudi nyumbani ilibidi nibebe mzigo niingie mtaani.”
Anasema aliendelea na kazi kwa wiki mbili kabla ya kufukuzwa. ”Nilifukuzwa kwa kuwa sikuwa na mkataba wowote wa kazi basi sikuweza kusaidiwa hata polisi nilikokimbilia.”
Wanasema ‘Ninaoongea kwa kuvibrate’
Rukia anasema kuwa anapolazimika kupiga simu watu husema, ”Hee unaongeaje hivyo kama unalia, mara unaongea kama unalazimishwa…hawaelewi kwamba ni kwa sababu ya tatizo la usikivu hafifu, nikiongea inasikika kama ina ‘vibrate’.
Anasema amekuwa akiwaelimisha wafuasi wake mtandaoni na wale anaokutana nao kuhusu hali ya usikivu hafifu na jinsi ya kuishi na watu wenye hiyo hali.
”Kuna baadhi ya watu wananitafuta wananiambia mwanangu hataki kujitokeza kufanya kazi kwa sababu watu wanambeza,” anasema Rukia ambaye hukutana na baadhi ya wazazi wenye vijana wenye ulemavu huo japo baadhi wamekuwa wakishindwa kujishughulisha kwa kuhofia kubezwa.

Chanzo cha picha, Rukia Jamal
Alipataje changamoto ya usikivu hafifu?
Rukia anaaeleza kwamba tatizo la usikivu hafifu hakuzaliwa nalo, bali baada ya kujifungua Januari 2018 ndipo kwa mara ya kwanza tatizo lilizidi na masikio kuziba kabisa. ”akiongea namsikia vizuri kuwa anaongea lakini siwezi kuelewa yale maneno”
Rukia anaeleza kwamba alifanya Jitihada za kutafuta ufumbuzi wa tatizo hili katika hospitali mbalimbali kama Muhimbili na KCMC ambako alishauriwa kutumia kifaa maalum cha kusaidia kusikia.
Nilijaribu kutumia hicho kifaa lakini hakikunisaidia nikaacha. Anaongeza.
Wataalamu wanasemaje?
Daktari bingwa wa magonjwa ya masikio, pua na koo, Chritopher Mwansasu anasema kuna uhusiano wa tatizo la usikivu hafifu na ujauzito.
‘’Kuna baadhi ya usikivu unaweza ukapungua kutokana na kupata ujauzito. Na kuna uhusiano wa karibu na ugonjwa unaoitwa Otosclerosic ambapo baadhi ya watu wakipata ujauzito, viungo vyao vya sikio la kati hushindwa kufanya kazi vizuri.
Aelezea mafaniko yake

Chanzo cha picha, Rukia Jamal
‘Kwanza ninajivunia namna ninavyojiamini’, anasema Rukia. Wapo wengi ambao wanashindwa kufanya mambo yao kwa sababu ya usikivu hafifu.
Rukia anasema watu wengine hawawezi hata kuhudhuria hafla na shughuli mbalimbali za kijamii.
Amesema pamoja na yote huhudhuria hafla mbalimbali kama kawaida hata kama hatasikia kila kitakachozungumzwa lakini ataambulia japo mawili.
‘Siku zote ni lazima kujichanganya na watu kwa sababu pesa zetu zote zipo kwa watu, nimeweza kufungua biashara yangu mwenyewe na kufuata bidhaa na kuwaagizia wengine bidhaa China’.
Anasema Mitandao ya kijamii imemsaidia kwa kiwango kikubwa, alianza kwa kuchukua picha za bidhaa kwenye maduka ya watu na kuchapisha mitandaoni.
Rukia anasema changamoto kubwa kwa wafanyabiashara wa mtandaoni ni wateja kutoamini, lakini kadri anavyochapisha matangazo kila siku bila kutokea malalamiko ya kutapeliwa ndivyo wateja wanavyozidi kumuamini.
Hadi sasa anayamudu maisha yake na wategemezi wake kupitia duka la manukato na kukodisha nguo za harusi.
Kama haitoshi anawafundisha pia wengine pia kuanza biashara kwa mtaji mdogo.