Chad yasitisha makubaliano ya kijeshi na Ufaransa
Chad yasitisha makubaliano ya kijeshi na Ufaransa

Chanzo cha picha, AFP
Chad imesema inasitisha makubaliano muhimu ya ushirikiano wa kiulinzi na Ufaransa, na hivyo kuzua maswali kuhusu kupungua kwa ushawishi wa Paris katika eneo linalokabiliwa na mzozo la Sahel barani Afrika.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Chad Abderaman Koulamallah alisema ni wakati wa nchi yake "kudai mamlaka yake kamili".
Tangazo hilo limekuja saa chache baada ya mwenzake wa Koulamallah wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, kukutana na Rais wa Chad Mahamat Deby.
Chad ni mshirika mkuu katika mapambano ya nchi za Magharibi dhidi ya wanamgambo wa Kikijihadi katika eneo la Sahel huko Afrika Magharibi.
Lakini kabla ya uchaguzi wa rais mwezi Mei, mamlaka ya Chad iliamuru kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani nchini humo, kuashiria kujiwtengai na washirika wa jadi wa nchi hiyo wa Magharibi.
Ufaransa kwa sasa ina takriban wanajeshi 1,000 katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati wanayotoa usaidizi wa kijasusi na vifaa kwa wanajeshi wa Chad kutoka katika kambi zao, ukiwemo katika mji mkuu N'Djamena.
Ufaransa, mtawala wa zamani wa kikoloni wa Chad, alikuwa ametia saini toleo lililorekebishwa la makubaliano ya kijeshi na usalama mnamo 2019.