Chama cha ACT wazalendo chataka uchaguzi wa serikali za mitaa urudiwe
Chama cha ACT wazalendo chataka uchaguzi wa serikali za mitaa urudiwe
Chama cha upinzani cha ACT Wzalendo nchini Tanzania kimetaka uchaguzi wa serikali za Mitaa urudiwe na matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya TAMISEMI kufutiliwa mbali.
"ACT hatukubaliani na matokeo yaliyotangazwa na Waziri wa TAMISEMI, kwani mchakato mzima wa uchaguzi umevurungwa kwa kiwango ambacho kimepora madaraka ya wananchi kuchagua viongozi wao,' imesema sehemu ya taarifa ya chama hicho.
Serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilitangaza matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika hivi karibuni, ambapo chama kinachoongoza nchi, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeshinda kwa asilimia 98.8, kikiibuka na ushindi wa nafasi 4,213 katika nafasi za serikali za mitaa.
Kwa upande mwingine, chama kikuu cha upinzani, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeshinda nafasi 36 pekee, sawa na asilimia 0.84 ya jumla ya nafasi zilizogombewa.
Matokeo hayo yanakuja baada ya malalamiko kutoka kwa baadhi ya vyama vya upinzani, wakiwemo viongozi wa Chadema, ambao wamekosoa mchakato wa uchaguzi.
Chadema inadai kwamba uchaguzi huo haukuzingatia misingi ya demokrasia, huku wakitaja kuwa baadhi ya wananchi walikosa haki ya kupiga kura kwa sababu ya kutokuwepo kwa majina yao kwenye daftari la wapigakura. Aidha, Chadema wameeleza kuwa baadhi ya wagombea wao walikumbwa na vitendo vya vurugu, wakiwemo viongozi wao waliouawa.