China yamfunga mwandishi wa habari aliyepatikana na hatia ya ujasusi

 

China yamfunga mwandishi wa habari aliyepatikana na hatia ya ujasusi

xx

Chanzo cha picha, Reuters

Mwanahabari wa zamani wa vyombo vya habari vya serikali ya China amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la ujasusi, familia yake imethibitishia kwa BBC.

Dong Yuyu, 62, ambaye amekuwa kizuizini tangu 2022, alikuwa akifanya kazi katika nchini Marekani na Japan na alikutana mara kwa mara na wanadiplomasia wa kigeni.

Alikuwa akila chakula cha mchana na mwanadiplomasia wa Japan mjini Beijing alipokamatwa na polisi.

Wakati wa kuzuiliwa kwake, Dong alikuwa mfanyakazi mkuu wa gazeti la Guangming Daily, mojawapo ya magazeti makuu matano yanayohusishwa na Chama cha Kikomunisti cha China.

Mnamo Februari 2022, Dong alikamatwa akiwa anakula chakula cha mchana na mwanadiplomasia wa Japan siku moja baada ya Michezo ya Olimpiki ya Majira ya baridi kumalizika huko Beijing, kwenye mgahawa ambapo mara nyingi alikuwa akikutana na marafiki wa kigeni.

Mwanadiplomasia huyo pia alizuiliwa - kisha akaachiliwa saa kadhaa baadaye huku kukiwa na maandamano kutoka kwa serikali ya Japan.