Daktari aangua kilio wakati anasimulia unyama wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza

 

Nov 29, 2024 11:42 UTC
  • Daktari aangua kilio wakati anasimulia unyama wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ghaza

Daktari Tanya Haj-Hassan, ameangua kilio katika mkutano wa Umoja wa Mataifa alipokuwa akisimulia tajiriba aliyopitia katika Ukanda wa Ghaza unaoendelea kushuhudia vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yanayofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa eneo hilo lililowekewa mzingiro.

Haj-Hassan ambaye alikuwa akihutubia kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Mshikamano na Watu wa Palestina inayoadhimishwa kila mwaka Novemba 29, amesimulia kumbukumbu za mateso wanayopata Wapalestina aliyoyashuhudia kwa macho yake wakati alipokuwa Ghaza.
 
Daktari Tanya Haj-Hassan amesema: "ninataka ulimwengu wote ujue kuwa baada ya yote, mimi ni mwanadamu, si kalamu iandikayo kwenye karatasi. Si kiumbe nisiyejulikana. Mimi ni mwanadamu niliyeumbwa na Mungu”.
 
Akizungumzia jinsi jamii ya kimataifa ilivyoyapokea maafa ya Wapalestina, daktari huyo amesema: "tumetumia miezi 14 iliyopita kutazama mauaji ya kimbari yaliyowahi kuakisiwa zaidi mubashara na kwa ushahidi kamili katika historia."
 
Bi Haj-Hassan amezishutumu taasisi za kimataifa na nchi za ulimwengu kwa kushindwa kuchukua hatua ipasavyo kwa ukiukaji mkubwa kupindukia wa sheria za kimataifa, ukiukaji wa haki za binadamu na uhalifu wa kivita.
 
Daktari huyo amesema, waliojionea kwa macho yao wameripoti uhalifu "ambao kama ungefanywa katika muktadha na sababu zingine zozote ungepeleka kuwekwa vikwazo," na akaongeza kuwa, mwitikio wa jamii ya kimataifa ni wa "kushindwa kuchukua hatua yoyote ya maana."
 
Aidha, Haj-Hassan amekosoa "kampeni za propaganda kubwa zinazofanywa kuhalalisha yasiyo na uhalali, kuwanyamazisha watu, na kuwadunisha wale ambao wamejaribu kufichua" jinai na uhalifu wa Israel.
 
Daktari huyo amesisitiza pia kwa kusema, iko siku atatokea mtu ambaye atazifukua rekodi na kumbukumbu zilizohifadhiwa na Wapalestina wenyewe zilizoangazia mauaji yao ya kimbari wakati waandishi wa habari wa kimataifa "walipopigwa marufuku kwa namna ambayo haijawahi kushuhudiwa".../