Emmanuel Wanyonyi: Kutoka kuchunga ng'ombe hadi kuwa bingwa wa Olimpiki
Emmanuel Wanyonyi: Kutoka kuchunga ng'ombe hadi kuwa bingwa wa Olimpiki

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa
- Author, Kelvin Kimathi
- Nafasi, BBC Sport Africa, Nairobi
Alikulia katika umaskini uliokithiri katika kijiji kidogo magharibi mwa Kenya, maisha ya kila siku ya Emmanuel Wanyonyi yalikuwa magumu.
Alipolazimika kuacha shule akiwa na umri wa miaka 10, alifanya kazi ya kulisha ng'ombe kwa muda mrefu. Wakati mwingine alipata chini ya $2 kwa mwezi.
Wanyonyi alivumilia mateso na kutumiwa vibaya, akibadili kazi mara kwa mara baada ya wakati mwingine kutolipwa, lakini mwanamume ambaye alikuja kuwa bingwa wa Olimpiki wa mita 800 alivumilia kwa sababu makazi na chakula vilitolewa.
"Maisha, na kuchunga ng'ombe kama mtoto, yalikuwa magumu," Wanyonyi aliambia BBC Sport Africa.
“Nilifikiria kuacha kazi hiyo na kurudi nyumbani lakini nikakumbuka kuwa bado ningekumbana na changamoto zile zile nilizokuwa nazikimbia.
"Nilipopata kitu kidogo, ningekipeleka nyumbani kwa ndugu zangu ili wapate chakula."
Mmoja wa watoto 11, Wanyonyi hakuwa na jingine ila kuacha shule kwani familia yake haikuweza kumudu karo ya mitihani ya shilingi 40 za Kenya ($0.30).
Hatimaye alifanikiwa kurejea na kuendelea na elimu na baadhi ya mapato yaliyokusanywa kama mchungaji wa mifugo na kwa kufanya vibarua na kugundua azma yake na uwezo katika riadha.
Kisha kikaja kifo cha ghafla na kisichoelezeka cha baba yake, ambaye alifanya kazi kama mlinzi kwenye bwawa, mnamo 2018.
"Alikuwa ametoka shuleni ili kunipa pesa za kununua viatu vya kukimbia na malipo aliyopata siku hiyo," Wanyonyi, ambaye sasa ana umri wa miaka 20, alieleza.
“Ni kana kwamba alinyongwa na kuwekwa kando ya maji, alikutwa na alama kichwani kana kwamba alipigwa.
"Ninachofikiri kilichotokea ni kwamba aliweka nguo zake huko kuogelea na kisha mtu akaja kumnyang'anya."
Bila uchunguzi rasmi wa maiti, Wanyonyi anasema familia yake "haijapata kufunga awamu hiyo ya maswali na majonzi".
"Siku hiyo, ulimwengu wangu ulisambaratika. Ilikuwa uchungu lakini sikuwa na muda wa kuhuzunika. Ilibidi niwe kiongozi wa nyumbani mara moja."
Kupanda kwa kasi kwa umaarufu

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa sababu babake hakuwepo, Wanyonyi alitarajia kuendeleza taaluma ya riadha ili kusaidia kukimu familia yake.
Lakini awali alikabiliwa na kejeli kwa sababu, tofauti na maeneo mengine ya Kenya, eneo la nyumbani kwake halijulikani kwa kutoa wakimbiaji mahiri.
"Wakati [Emmanuel] alipokuwa akikimbia, watu walikuwa wakimdhihaki na kumcheka," mamake Wanyonyi Margaret Nasimiyu alikumbuka.
"Nilikuwa nikilia na kuhuzunishwa na jambo hilo, lakini kijana wangu aliniambia: 'Usilie mama. Siku moja nitakununulia ardhi na utaishi maisha mazuri'.
"Nilidhani ni mzaha tu, lakini Mungu alikuwa pamoja naye."
Kufuatia kurejea shuleni, Wanyonyi hakuwa na pesa za viatu vya kukimbia.
"Kama ningepata viatu, ningefanya mazoezi. Kama sivyo, ningekimbia bila viatu mashambani," aliongeza.
"Wakati mwingine viatu vingekatika siku moja na ningelazimika kusubiri hadi nipate jozi nyingine. Lakini sikuruhusu hilo kunizuia."
Hata hivyo, Wanyonyi anasifu miaka yake ya utotoni - na masuala aliyoshinda - akisema yalimimarisha kiakili.
"Hakuna changamoto katika maisha ambayo inaweza kunishtua," alisema.
"Watu waliponitilia shaka au kunicheka, sikuiruhusu kunivunja."
Ushindi wa Olimpiki huko Paris

Chanzo cha picha, Getty Images
Kujituma kwa Wanyonyi na ushupavu wake ulivutia macho ya walimu wake, na akaanza kushiriki mashindano ya kanda nchini Kenya.
Akivutia kwa kasi yake na ustahimilivu, licha ya ukosefu wa mafunzo rasmi, alipanda haraka akisajili msururu wa ushindi.
“Watu waliendelea kuniambia, ‘Unaweza kufika mbali, Emmanuel’ lakini sikuamini,” alisema.
"Sikujiona kama kitu maalum. Nilikuwa nakimbia tu."
Mnamo Juni mwaka huu, akiwa bado na umri wa miaka 19, Wanyonyi alikuwa mkimbiaji wa tatu kwa kasi wa mita 800 wa wakati wote katika majaribio ya Olimpiki ya Kenya.
Kisha akafuata hilo kwa kushinda medali ya dhahabu huko Paris 2024 mnamo Agosti.
"Sio taji pekee - Lina umuhimu mkubwa katika maisha yangu," Wanyonyi alisema.
"Laiti baba yangu angekuwa hapa anione nikikimbia. Ningejisukuma zaidi kwa sababu yake, kwa sababu ya upendo aliokuwa nao kwangu."
Kocha wa Wanyonyi Claudio Berardelli amemsifu kama "talanta ya ajabu".
"Ana mchanganyiko wa kipekee wa kasi na ustahimilivu," Muitaliano huyo aliiambia BBC Sport Africa.
Kulenga rekodi ya dunia

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa
Huku medali ya dhahabu ya Olimpiki ikiwa tayari imepatikana mapema sana katika taaluma yake, matarajio ya Wanyonyi yameongezeka.
Malengo yake ni kuvunja rekodi ya dunia ya mita 800 ya dakika moja na sekunde 40.91, ambayo iliwekwa na Mkenya mwenzake David Rudisha kwenye Michezo ya Olimpiki ya London 2012.
Wanyonyi alikuwa tu sehemu ya kumi ya sekunde ya punguzo katika mkutano wa Diamond League huko Lausanne mnamo Agosti.
"Ana uwezo huu wa kuendelea kusukuma wengine wanapoanza kufifia," Beradelli alisema.
Muitaliano huyo analeta uzoefu wake mwenyewe, akiwa amewahi kufanya kazi na mabingwa watatu wa dunia wa 800m.
Maendeleo katika teknolojia ya michezo, kuanzia nyanja za riadha hadi viatu, yanaweza kumsaidia Wanyonyi katika harakati zake za kufikia rekodi hiyo, huku uwezo wake wa kiakili ukiwa muhimu.
"Wanyonyi ni bingwa akilini mwake," kocha wake alibainisha.
“Hana woga pengine kutokana na historia yake, hata anapokuwa na siku ngumu huwezi kumuona akipoteza matumaini.
"Anajua daima kuna siku mpya ya kujaribu tena. Hilo ndilo linalomtofautisha na wengine."
Kuboresha maisha ya familia

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa
Kwa Wanyonyi, kuvunja rekodi ya dunia ni zaidi ya kuweka tu muda
"Nataka kuacha urithi," alisema kwa uamuzi wa utulivu.
"Sijatekwa nyara na hatua hiyo, lakini naamini inawezekana. Najua kuna kiwango natakiwa kufikia na bado sijafika."
Mafanikio yake yamemwezesha kuboresha hali ya familia yake, kujenga nyumba za vyumba vitatu kwa ajili ya mama yake na kaka zake watatu, na kulipia karo za shule kwa wadogo zake wanne.
"Nilitaka kufanya kile ambacho baba yangu angewafanyia," alisema.
"Walipaswa kujua kwamba hawakuwa peke yao."
Anapojiandaa kwa msimu wa 2025 - na hatimaye kutafuta rekodi ya dunia - familia ya Wanyonyi inasalia kuwa motisha yake kuu.
“Nikiitazama familia yangu na tulikotoka inanipa nguvu tu, sipati usingizi na siwezi kupumzika,” alisema.
"Wamepitia mengi na ninataka kuwapa maisha bora."