Israel yaonya raia dhidi ya kurejea katika vijiji 60 vya Lebanon
Israel yaonya raia dhidi ya kurejea katika vijiji 60 vya Lebanon
Jeshi la Israel limewaonya raia wa Lebanon kutorejea katika vijiji 60 kusini mwa nchi hiyo, siku tatu baada ya kusitishwa kwa mapigano baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mapigano na kundi la wapiganaji la Shia la Hezbollah.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilichapisha ramani inayoonyesha eneo lenye kina cha maili kadhaa, ambalo lilisema wakazi hawapaswi kurudi. Yeyote atakayefanya hivyo, lilisema, atakuwa anajiweka hatarini.
Zaidi ya Walebanon milioni moja wamekimbia makazi yao kutokana na mapigano hayo, wengi wao kutoka kusini. Makumi ya maelfu ya Waisraeli pia wameyakimbia makazi yao.
Usitishaji wa mapigano ulianza kutekelezwa Jumatano asubuhi, ingawa maafisa wa Israeli na Lebanon wameshtumu kila mmoja kuwa tayari amekiuka.
Siku ya Alhamisi, IDF ilisema vikosi vyake vilifyatua mizinga na kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya wappiganaji kusini mwa Lebanon.
Iliongeza kuwa iliwafyatulia risasi washukiwa baada ya kuona shughuli katika kituo cha silaha cha Hezbollah, na magari yakiwasili katika maeneo kadhaa, ambayo ilisema yalikiuka usitishaji mapigano.
Lebanon iliishutumu Israel kwa kukiuka makubaliano "mara kadhaa" na kusema inafuatilia hali hiyo.