Khatibu wa Sala ya Ijumaa: Magharibi iwezeshe kufanyika mazungumzo kwa kuheshimu haki za taifa la Iran
Khatibu wa Sala ya Ijumaa: Magharibi iwezeshe kufanyika mazungumzo kwa kuheshimu haki za taifa la Iran
Nov 29, 2024 12:08 UTC
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesema: "ikiwa Magharibi itarekebisha mwenendo wake na pande mbili zikaheshimiana, itaweza kuandaa mazingira ya kufanyika mazungumzo na kufikia makubaliano na Iran".
Hujjatul-Islam Wal-Muslimin Mohammad Hasan Abu Turabi Fard
amesema Iran yenye nguvu daima iko tayari kwa majadiliano na mazungumzo
ya kimantiki na ya kielimu, na akaongezea kuwa, ikiwa Magharibi
itarekebisha mwenendo wake na pande mbili zikaheshimiana; na ikazingatia
haki za taifa adhimu na lenye nguvu la Iran itaweza kuandaa mazingira
ya kufanywa mazungumzo na kufikia makubaliano.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya Tehran ameongeza kuwa: Umoja wa Ulaya
haunufaiki na sifa ya kuwa taasisi huru na inayojitegemea, kwa sababu
maslahi ya Ulaya yamefanywa mhanga wa uchu wa Marekani; na kwa upande
mwingine, sera za upendeleo zinazofuatwa katika eneo la Asia
Magharibi ni miongoni mwa sababu za kushindikana kujengwa uhusiano
thabiti na endelevu na Iran kwa muda wote wa miongo minne sasa.
Akiashiria hatua isiyo ya kawaida na ya kiuadui ya Umoja wa Ulaya
ya kutoa taarifa ya pamoja na nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano wa
Ghuba ya Uajemi na kuzusha madai yasiyo na msingi kuhusiana na visiwa
vitatu vya Iran, Hujjatul-Islam Abu Turabi Fard amesisitiza kuwa: nchi
za Magharibi zimepata tajiriba ya matukio mawili ya uhalisia katika
miongo michache iliyopita; la kwanza ni kwamba, masuala ya eneo la
kistratejia la Asia Magharibi hayataweza kutatatuliwa kamwe bila ya
kuzingatia maslahi na msimamo wa Iran; na la pili, haiwezekani kuingia
katika mazungumzo na Iran yenye nguvu kwa kutumia wenzo wa mashinikizo
na vitisho.
Khatibu wa Sala ya Ijumaa ya mjini Tehran ameendelea kusisitiza
kuwa, nguvu za Muqawama zimewapigisha magoti Wazayuni; na Wazayuni hao
hawakuweza kufikia malengo yao yoyote nchini Lebanon; na akaongeza kuwa:
Iran ya Kiislamu inajivunia kwamba imekuwa na itaendelea kuwa pamoja na
taifa adhimu la Lebanon katika hali zote za shida na raha; na ushindi
huo mkubwa kwa mara nyingine tena umedhihirisha kushindwa mashine ya
vita ya utawala wa Kizayuni mbele ya macho ya jamii ya kimataifa.../