Kwa nini ndege zisizo na rubani zinapaa karibu na vituo vya kijeshi vya Marekani, nchini Uingereza?
Kwa nini ndege zisizo na rubani zinapaa karibu na vituo vya kijeshi vya Marekani, nchini Uingereza?
Eneo la anga karibu na vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyoko Norfolk na Suffolk limekuwa likichunguzwa kufuatia matukio kadhaa ya hivi karibuni ya uvamizi wa ndege zisizo na rubani. Wanaohusika na ndege hizo bado hawajapatikana na wakazi wa maeneo ya karibu wamehoji kwa nini matukio haya yameruhusiwa kufanyika.
Matukio ya uvamizi wa ndege zisizo na rubani yaliripotiwa kwa mara ya kwanza katika vituo vitatu vya kijeshi vya Marekani – RAF Mildenhall na RAF Lakenheath huko Suffolk, pamoja na RAF Feltwell huko Norfolk, kati ya tarehe 20 na 22 Novemba, na ndege hizo zimeonekana tena.
Kijijini cha Beck Row, Suffolk, ambacho kipo karibu na RAF Mildenhall, wakazi wake waliripoti kuona vyombo vya angani vyenye mwanga mkali vikielea juu ya nyumba zao na juu ya kambi hiyo.
'Kwanini wanaziruhusu ndege hizi kuzunguka hapa?'
Casseem Campell, mwenye umri wa miaka 28, alisema ameona kitu juu ya nyumba yake huko Beck Row.
Alielezea kuona chombo cha anga chenye umbo la pembetatu, kilicho na rangi ya "kijivu, nyeusi," katika moja ya matukio mawili ya ndege zisizo na rubani aliyoyaona jioni katika wiki iliyopita.
"Zilikuwa na kelele kubwa na taa. Kusema kweli, zilionekana kuwa rasmi," aliongeza.
"Ikiwa ni tishio, kwa nini hazitunguliwi? Kwa nini ziruhusiwe kuruka ikiwa zina nia mbaya?"
Tangu wakati huo imebainika kuwa droni moja ilikaribia umbali wa yadi 273.40 (mita 250) kutoka HMS Queen Elizabeth, meli kuu ya kubeba ndege ya Royal Navy, ilipoingia Bandari ya Hamburg tarehe 22 Novemba.
RAF Fairford huko Gloucestershire, ambapo mabomu ya Marekani ya B-52 yalikuwa yametumwa hivi karibuni, pia iliripoti tukio la hivi karibuni.
Wanajeshi wa Uingereza wamepelekwa kusaidia juhudi za Marekani kuwasaka waliohusika.
'Polisi wamekuwa wengi'
Chrystal Mason, mwenye umri wa miaka 28, alisema ameona droni mbili wiki iliyopita huko Beck Row.
Binti wa kambo wa rubani wa RAF, alielezea kuona mpira wa rangi ya machungwa angani majira ya usiku pamoja na kuongezeka kwa shughuli katika kituo cha kijeshi cha Marekani.
"Katika siku 10 zilizopita, nimeona magari ya kijeshi yakiwa karibu na kijiji. Kumekuwa na uwepo mkubwa zaidi wa polisi kuliko kawaida ;wanajeshi na polisi wa Uingereza," alisema.
Bi Mason pia alielezea kile alichoamini kuwa ni droni ikizuiwa, ingawa BBC haikuweza kuthibitisha hili.
"Kulikuwa na mwanga mkubwa wa rangi ya machungwa angani na ghafla ukatoweka. Nilisikia watu wakipiga kelele 'wow'," aliongeza mama wa mtoto mmoja.
'Nimeziona droni mara tatu au nne'
Johnny Whitfield, ambaye pia anaishi huko Beck Row, alieleza jinsi kulivyokuwa na "shughuli nyingi."
"Nimeona ndege zisizo na rubani mara tatu au nne," alisema, kabla ya kuthibitisha kuwa matukio hayo yalitokea majira ya usiku ,wiki iliyopita.
Pia alielezea kuona vitu vikiruka angani vikiwa na taa na vikielea juu ya kituo cha kijeshi, ingawa alisema hakuweza kujua ni kelele za nini , huku akisema vyombo hivyo vilikuwa vikubwa.
"Unachoona ni mwanga tu, lakini ni mwanga mkubwa sana," aliongeza.
Alisema alihisi kuwa jeshi la Marekani halikuwa wazi kuhusu kinachoendelea.
"Huwezi jua kama ni wageni au wakazi . [Jeshi la Anga la Marekani] halijatoa taarifa zaidi kuhusiana na tukio hilo.
"Unapata taarifa zaidi kutoka Facebook kuliko kutoka kwa kambi."
Ndege zilizolazimika kubadili uwelekeo
Wakazi wa Beck Row waliokutana na BBC walielezea ongezeko la shughuli za kijeshi katika eneo hilo, huku kukiwa na ongezeko la ndege angani.
BBC pia imeshuhudia maafisa kutoka Ofisi ya Uchunguzi Maalum wa Jeshi la Anga la Marekani walikuwa katika eneo la Suffolk na walizungumza na wakazi wa eneo hilo kuhusu kile walichokiona.
Roger Smith, mtaalamu wa masuala ya anga ya kijeshi kutoka Suffolk, aliambia BBC kuwa aliamini rubani wa Jeshi la Anga la Marekani walirudi kwa njia za mawasiliano salama zaidi siku za karibuni.
"Sasa wanatumia kiungo cha data kilichosimbwa badala ya redio wanapozungumza " alisema.
Hata hivyo Uwanja wa Ndege wa Glasgow Prestwick au Jeshi la Anga la Marekani hawakutoa maoni kuhusu madai hayo.
Hatua za kisheria kuchukuliwe
Vyanzo vya ulinzi vimeambia BBC kuwa kuna wasiwasi kuwa yawezekana mtumishi wa umma" anahusika na uvamizi huo.
Hadi sasa, mamlaka za Marekani na Uingereza hazijaweza kusema ni nani anayehusika.
Waziri wa Ulinzi Lord Coaker aliiambia Bunge la Lords Alhamisi: "Wizara ya Ulinzi inafahamu kuhusu taarifa hizi na inashirikiana kwa karibu na vikosi vya Marekani vinavyotembelea, polisi wa kwenye makazi yao na washirika mengine kusaidia katika matukio ya hivi karibuni.
"Tunaichukulia kwa uzito suala lolote la usalama na tunachukua hatua madhubuti kwenye maeneo ya Wizara ya Ulinzi. Hii inajumuisha uwezo wa kukabiliana na drones."
Waziri aliiambia Bunge: "Ni kinyume cha sheria kurusha drones au kuwa katika maeneo ya karibu na vituo hivi vya kijeshi, na watu wanapaswa kuwa na ufahamu wa hilo."
"Suala hili bado linnaoendelea kufanyiwa uchunguzi."
Awali, Wizara ya Ulinzi, inayomiliki vituo vya kijeshi, ilisema: "Tunachukulia vitisho kwa uzito na tunadumisha hatua madhubuti kwenye maeneo ya ulinzi."
Jeshi la Anga la Marekani huko Ulaya lilisema: "Hadi sasa, viongozi wa vituo wameamua kwamba hakuna uvamizi ulioathiri wakazi wa kambi, vifaa au mali."
Jeshi la Anga linachukua hatua zote zinazohitajika kulinda vituo na wakazi wake."