Macron akiri ilichofanya Ufaransa 1944 kwa askari wa Afrika Magharibi ni "mauaji ya halaiki"

 

Nov 29, 2024 11:41 UTC
  • Macron akiri ilichofanya Ufaransa 1944 kwa askari wa Afrika Magharibi ni

Kwa mara ya kwanza, Rais wa Ufaransa ameyatambua mauaji ya wanajeshi wa Afrika Magharibi yaliyofanywa na Jeshi la Ufaransa mwaka 1944 kuwa ni "mauaji ya halaiki. Macron amechukua hatua hiyo kupitia barua aliyoziandikia Mamlaka za Senegal.

Hayo yamethibitishwa na Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal katika kipindi cha mahojiano aliyofanyiwa na televisheni ya taifa ya Ufaransa kilichorushwa hewani jana Alkhamisi.
 
Hatua ya Macron inakuja katika mkesha wa kuadhimisha miaka 80 ya mauaji ya Vita vya Pili vya Dunia huko Thiaroye - kijiji cha wavuvi nje kidogo ya mji mkuu wa Senegal, Dakar.
 
Waafrika Magharibi walikuwa askari wa kitengo kilichoitwa Tirailleurs Senegalais, kikosi cha askari wa miguu katika Jeshi la kikoloni la Ufaransa.
 
Kati ya wanajeshi 35 na 400 wa Afrika Magharibi waliopigania Jeshi la Ufaransa katika Vita vya Ufaransa mwaka 1940 waliuawa Desemba 1, 1944 na wanajeshi wa Ufaransa baada ya kile kilichoelezwa kuwa ni maasi ya kutolipwa mishahara.
 
Baadhi ya wanajeshi walioandamana walishtakiwa mnamo Machi 1945.
 
Faye amesema hatua hiyo ya Macron inapasa "kufungua mlango" ili "ukweli wote kuhusu tukio hilo chungu la Thiaroye" uweze kuwekwa wazi.
 
Rais wa Senegal ameongezea kwa kusema: "kwa muda mrefu tumetafuta njia ya kuhitimisha hadithi hii na tunaamini kwamba, wakati huu, ahadi ya Ufaransa itakuwa kamili, ya moyo safi na ya ushirikiano".
 

Sehemu moja ya barua ya Macron imesema: "Ufaransa lazima itambue kwamba siku hiyo, makabiliano kati ya wanajeshi na wabeba bunduki waliotaka walipwe mishahara yao halali, yalizua mlolongo wa matukio ambayo yalisababisha mauaji".

Rais wa Ufaransa ameongezea kwa kusema: "pia ni muhimu kubainisha, kadiri inavyowezekana, sababu na ukweli uliosababisha janga hili, nimeziomba taasisi zangu zinijulishe maendeleo ya kazi ya Kamati ya Mrejesho wa Ukweli, ambao serikali yako imeamua kuanzisha, chini ya uongozi wa Profesa Mamadou Diouf, ambaye hadhi na sifa zake zinatambuliwa na wote".

Ufaransa ingali ina wanajeshi wapatao 350 katika koloni lake la zamani la Senegal, ambao zaidi wanatoa mchango wa usaidizi.

 Alipoulizwa kuhusu uwepo wa askari hao, Faye amedokeza kwamba haitakuwa kitu ambacho Wasenegali wangekitaka.

Amefafanua kwa kusema: "ni wazi kabisa; nadhani ukibadilisha kidogo tu nafasi, utakuwa na wakati mgumu kufikiria kwamba (ikubalike) jeshi jengine, liwe la China, Russia, Senegal, au nchi nyingine yoyote kuwa na kambi ya kijeshi huko Ufaransa".../