Mashirika ya misaada yasitisha shughuli Gaza baada ya wafanyakazi kuuawa kwa shambulizi la Israel
Mashirika ya misaada yasitisha shughuli Gaza baada ya wafanyakazi kuuawa kwa shambulizi la Israel
Shirika la kutoa misaada la World Central Kitchen (WCK) limesema kuwa linasitisha shughuli zake huko Gaza baada ya gari lililokuwa limebeba wafanykazi wake kupigwa na shambulio la anga la Israel.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilisema mlengwa wa shambulizi hilo alishiriki katika mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israeli, na kwa sasa ameajiriwa na WCK.
WCK ilisema "imesikitishwa" kwamba gari lililokuwa limebeba wafanyakazi lilipigwa na ilikuwa ikitafuta maelezo zaidi, ingawa iliongeza "haijui" kwamba mtu yeyote kwenye gari alikuwa na uhusiano na shambulio la Oktoba 7.
Shirika la habari la serikali ya Palestina, Wafa liliripoti kuwa watu watano waliuawa katika shambulio hilo huko Khan Younis, kusini mwa Gaza, siku ya Jumamosi, na watatu kati yao wakiwa wafanyakazi wa WCK.
Walijumuisha mkurugenzi wa jikoni za WCK huko Gaza, shirika liliongeza.
Kando na hilo, shirika la misaada la Uingereza Save the Children lilisema mmoja wa wafanyakazi wake pia aliuawa Jumamosi alasiri huko Khan Younis.
Ahmad Faisal Isleem Al-Qadi, 39, alikuwa akirejea nyumbani kwa mkewe na bintiye wa miaka mitatu kutoka msikitini alipouawa, shirika la misaada liliongeza.
"Ahmad, ambaye alikuwa kiziwi, atakumbukwa kwa uamuzi wake wa kusaidia wengine, kwa fahari yake kwa binti yake, na kwa uwezo wake wa kufurahisha wengine,"
Save the Children ilisema katika taarifa. Haijulikani ikiwa aliuawa katika shambulizi kama ilivyokuwa kwa wafanyakazi wa WCK.
Shirika la Save the Children linasema kulikuwa na mashambulizi mawili mjini Khan Younis siku ya Jumamosi, lakini BBC haijaweza kuthibitisha hili.