Russia: Marekani na Uingereza zinaeneza machafuko ndani ya Syria kupitia magenge ya kigaidi
Russia: Marekani na Uingereza zinaeneza machafuko ndani ya Syria kupitia magenge ya kigaidi
Nov 29, 2024 11:41 UTC
Russia imesema madola makubwa ya Magharibi yanayoongozwa na Marekani yanaendelea na vitendo vyao vya chuki dhidi ya Syria kwa kuwaunga mkono wanamgambo wanaoipinga serikali ya Damascus pamoja na makundi ya kigaidi ya kitakfiri katika kila pembe ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova
amezikosoa Marekani, Uingereza na baadhi ya nchi nyingine za Magharibi
kwa kueneza machafuko katika kila pembe ya Syria kupitia makundi ya
kigaidi.
Zakharova ameongeza kuwa, uungaji mkono wa serikali za Magharibi
kwa makundi ya kigaidi yanayoendesha harakati zao katika kila pembe ya
Syria si jambo lililobaki kuwa siri bali limeshafichuliwa na liko wazi
hadharani.
Amesema: "majaribio ya kulilenga taifa la Syria, mamlaka yake ya
kujitawala na uhuru wake yamekuwa yakiendelezwa kwa miaka mingi na
serikali zinazochukia amani na usalama wa kimataifa kwa ujumla, na
zimeichagua Syria na zingali zinaendelea kuing'ang'ania na kuiandama kwa
uchokozi na uvamizi wao unaoendelea".
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Russia amebainisha kuwa
msimamo wa Moscow wa kuendelea kuiunga mkono Syria na watu wake umekuwa
msingi wa kudhamini usalama na utulivu katika eneo la Asia Magharibi.
Zakharova ametoa matamshi hayo baada ya ndege za Syria na Russia
kushambulia kwa mabomu maficho ya wanamgambo ili kuwarudisha nyuma
magaidi wa kitakfiri wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni na wanamgambo
wanaoipinga serikali ya Damascus katika eneo la kaskazini magharibi mwa
nchi hiyo.
Jeshi la Syria limesema linashirikiana na Russia na "vikosi rafiki"
kurejesha udhibiti wa maeneo na hali ya mambo kama ilivyokuwa hapo
awali.
Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi hilo, katika msururu wa operesheni
za mashambulio walizofanya, askari wa Syria wamewatia hasara
kubwa wanamgambo wa kitakfiri wanaoendesha harakati zao katika eneo hilo
la kaskazini magharibi mwa nchi.../