Wanajeshi wa Syria waondoka Aleppo huku waasi wakisonga mbele
Wanajeshi wa Syria waondoka Aleppo huku waasi wakisonga mbele
Majeshi ya serikali ya Syria yameondoka katika mji wa Aleppo baada ya mashambulizi ya waasi wanaopinga utawala wa rais Bashar al-Assad.
Jeshi lilikiri kwamba waasi walikuwa wameingia "sehemu kubwa" ya mji huo, ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini humo, lakini wakaapa kufanya mashambulizi ya kukabiliana.
Mashambulizi hayo yanaashiria mapigano makubwa zaidi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria katika miaka ya hivi karibuni.
Zaidi ya watu 300, wakiwemo takribani raia 20, wameuawa tangu ilipoanza siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Shirika la Kuchunguza Haki za Kibinadamu la Syria (SOHR) lenye makao yake nchini Uingereza.
Akizungumza siku ya Jumamosi, Rais Assad aliapa "kulinda uthabiti [wa Syria] na uadilifu wa eneo lake mbele ya magaidi wote na wanaowaunga mkono".
"[Nchi] ina uwezo, kwa usaidizi wa washirika na marafiki zake, kuwashinda na kuwaondoa, bila kujali mashambulizi yao ya kigaidi ni makali kiasi gani," ofisi yake ilimnukuu akisema.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimesababisha vifo vya takribani watu nusu milioni, vilianza mwaka 2011 baada ya serikali ya Assad kujibu maandamano ya kuunga mkono demokrasia.
Mzozo huo umesimama kwa kiasi kikubwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2020, lakini vikosi vya upinzani vimedumisha udhibiti wa mji wa kaskazini-magharibi wa Idlib na sehemu kubwa ya mkoa unaozunguka.
Idlib iko kilomita 55 tu kutoka Aleppo, ambayo yenyewe ilikuwa ngome ya waasi hadi ilipodhibitiwa na vikosi vya serikali mwaka 2016.