2024 watajwa kuwa mwaka mbaya zaidi kwa watoto kwenye mizozo duniani katika historia ya UNICEF


  • 2024 watajwa kuwa mwaka mbaya zaidi kwa watoto kwenye mizozo duniani katika historia ya UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limesema, zaidi ya watoto milioni 473, sawa na zaidi ya mtoto mmoja kati ya sita duniani kote anaishi kwenye vita, huku dunia ikigubikwa na mizozo mingi zaidi tangu kumalizika kwa Vita Kuu vya Kwanza vya Dunia.

Taarifa iliyotolewa leo na UNICEF imebainisha kuwa, asilimia ya watoto wanaoishi kwenye mizozo imeongezeka maradufu kutoka asilimia 10 miaka ya 1990 hadi asilimia 19 hivi sasa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwaka huu kuliko wakati wowote ule, watoto wengi zaidi wanakadiriwa kuwa wanaishi kwenye maeneo yenye mizozo au wamelazimika kukimbia makwao kutokana na mizozo.

“Idadi kubwa ya watoto waliodhurika na mizozo, haki zao zinakiukwa, ikiwemo kuuawa au kujeruhiwa, hawaendi skuli, wanakosa chanjo muhimu, na hawana lishe ya kutosha,” imesema taarifa hiyo ikisisitiza kuwa 2024 ni mwaka ambao UNICEF katika historia yake haijawahi kushuhudia kiasi hiki cha madhila yanayowafika watoto walioko kwenye maeneo yenye mizozo.

Kwa mujibu wa UNICEF, hadi mwishoni mwa mwaka 2023, watoto milioni 47.2 walikuwa wamefurushwa makwao kutokana na mizozo na ghasia, huku mwelekeo wa mwaka 2024 ukiashiria nyongeza zaidi ya watoto waliofurushwa kutokana na mizozo kushamiri Palestina, Lebanon, Sudan, Haiti na Myanmar.

Asilimia 30 ya wakazi wa dunia ni watoto, huku wakiwa asilimia 40 ya wakimbizi wote na asilimia 49 ya wakimbizi wa ndani.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Catherine Russell amenukuliwa kwenye taarifa hiyo akisema “kwa takribani kila kipimo, mwaka 2024 umekuwa mwaka mbaya zaidi kwa watoto walioko kwenye maeneo yenye mizozo”.../