Gaza: Hospitali kuu ya Kamal Adwan sasa 'haifanyi kazi'

Huko Gaza, hospitali muhimu kwa wakazi wa kaskazini mwa eneo hilo imeharibiwa sana wakati wa shambulio la Israeli. Kulingana na Shirika la Afya Duniani, WHO, imebidi kufungwa.

Huko Gaza, hospitali ya Kamal Adwan imeharibiwa vibaya wakati wa shambulio la Israeli. Hapa, ilikuwa Oktoba 31, 2024.
Huko Gaza, hospitali ya Kamal Adwan imeharibiwa vibaya wakati wa shambulio la Israeli. Hapa, ilikuwa Oktoba 31, 2024. AFP - -
Matangazo ya kibiashara

Shirika la Afya Duniani limesema operesheni ya kijeshi ya Israeli karibu na Hospitali ya Kamal Adwan imeifanya hospitali hiyo, ambayo ni kituo cha mwisho kikubwa cha afya kaskazini mwa Gaza, kusitisha huduma zake.

Maafisa wa wizara ya afya ya Gaza wameripoti kwamba wanajeshi wa Israel walivamia na kuchoma moto moja ya hospitali chache zilizosalia Gaza Kaskazini, baada ya kuwafukuza wafanyakazi wa hospitali na wagonjwa waliokuwepo.

Wanajeshi wa Israeli walivamia na kuchoma moto Hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Gaza, baada ya kuwaondoa kwa nguvu wagonjwa na wafanyakazi, Wizara ya Afya ya Gaza imesema, huku jeshi la Israeli likidai hospitali hiyo ilitumika na wapiganaji wa Hamas kama kituo, bila kutoa ushahidi.

Hata hivyo jeshi la Israeli lilikanusha kuwajibika moja kwa moja kwa moto mkubwa uliotekeza hospitali hiyo, likisema ni jengo tupu lililoathirika.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Hamas, jeshi la Israel lilivamia hospitali hiyo na kuwalazimu wagonjwa na wauguzi kukusanyika uani na kumvua nguo kutokana na baridi kali. Wakati Israel ilisema kwamba kabla ya kuzindua operesheni karibu na hospitali, wanajeshi wake "wamewezesha uhamishaji salama wa raia, wagonjwa na wafanyikazi wa matibabu".

Kamal Adwan ilikuwa hospitali ya mwisho ambayo bado inafanya kazi kaskazini mwa Gaza.

Ripoti kutoka Wizara ya Afya ya Gaza zinaonyesha kuwa zaidi ya Wapalestina 45,400 wameuawa tangu kuanza kwa vita vya Israel dhidi ya Hamas. Zaidi ya nusu ya vifo hivi ni wanawake na watoto, hali inayozidisha machungu katika jamii ya Gaza.

Vita hivi vilianzishwa na Hamas mnamo Oktoba 7, 2023, baada ya shambulio lao kusini mwa Israel ambalo liliua watu takriban 1,200 na kuwachukuwa mateka watu 250.

Hadi sasa, mateka 100 bado wanashikiliwa Gaza, ingawa ni theluthi mbili tu ya idadi hiyo wanaoaminika kuwa hai. Hali hii imezidi kuibua maswali kuhusu mustakabali wa ukanda huo na mateso yanayoendelea.