Intelijensia ya Russia: US na UK zinapanga mashambulio ya kigaidi dhidi ya vituo vyetu vilivyoko Syria
Idara ya Intelijensia ya Russia ya Nje ya Nchi (SVR) imetahadharisha kuwa Marekani na Uingereza zinapanga mashambulizi ya kigaidi katika vituo ya kijeshi vya nchi hiyo vilivyoko Syria ili hali ya nchi hiyo isitangamae na amani na uthabiti usirejee nchini humo.
Taarifa ya taasisi hiyo ya Intelijensia ya Russia imeendelea kueleza: "kwa mujibu wa taarifa zilizopo, wawakilishi wa Shirika la Ujasusi la Uingereza MI6 na la Marekani, CIA hivi majuzi waliwapa kazi makamanda wa IS walio chini ya udhibiti wao kutekeleza mfululizo wa mashambulizi kwenye kambi za kijeshi za Russia. Ili kufanya kazi hii chafu, magaidi hao wamepatiwa droni za mashambulizi".
SVR imesema: ili kuficha ushiriki wao katika mashambulizi hayo yaliyopangwa dhidi ya vituo vya kijeshi vya Russia, kamandi za kijeshi za Marekani na Uingereza zimeviagiza vikosi vyao vya anga kuendelea kufanya mashambulizi dhidi ya maeneo ya IS nchini Syria lakini kwa kutoa onyo na tarifa kabla kwa magaidi hao.
Kwa mujibu wa Idara ya Intelijensia ya Russia ya Nje ya Nchi, London na Washington zina tamaa kwamba chokochoko kama hizo zitaifanya Russia iwahamishe wanajeshi wake kutoka Syria na wakati huo huo, mamlaka mpya za Syria zitashutumiwa kwa kushindwa kuwadhibiti watu wenye misimamo na itikadi kali.../