'Kuanguka kwa Assad kulivyofungua sehemu ya maisha ya mume wangu ambayo sikuijua'

'Kuanguka kwa Assad kumenifanya kufahamu maisha ya zamani ya mume wangu ambayo nilikuwa sifahamu.'
Ilikuwa mwanzoni mwa mwezi Desemba pale Douna Haj Ahmed, mkimbizi kutoka Syria alipogundua taarifa mbaya zinazohusiana na kushikiliwa kwa mume wake katika gereza lenye sifa mbaya la Al-Khatib, linalofahamika kama "Jehanam ya Duniani".
Alikuwa akitazama jinsi wafungwa waliochanganyikiwa wakijaribu kuondoka katika moja ye eneo lenye ulinzi mkali, akiwa nyumbani kwake mjini London, baada ya vikosi vya waasi kumuondoa rais Bashar al-Assad kwenye nafasi yake kama rais.
Akiwa analia, Abdullah Al Nofal, mume wake wa miaka nane alikaa pembeni yake, na kumuangalia akisema "Hapa ndipo nilipokamatwa, Ni eneo hili."
Douna, ambaye kaka zake pia walikamatwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa muda wa miaka 13, anasema alikuwa ana uelewa wa kile ambacho mume wake alipitia wakati ameshikiliwa – lakini hii ilikuwa ni mara ya kwanza anamuelezea kiundani zaidi kuhusu kile alichokipitia.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Abdullah, hapendi kuonyesha hisia zake, anapenda kuonekana kama yeye ni jasiri sana kila wakati," Douna,33, aliiambia BBC.
"Ilikuwa ni wakati wa mabadiliko kwake. Nilimuona akiwa hana ujasiri. Nilimuona akiwa analia. Pengine ningekuwa mmoja wao sasa hivi, au ningekuwa nimekufa."
"Nahisi alipoona hii, alijihisi kama hii itakuwa namna ya yeye kukubaliana na hali na kufunga ukurasa huo wa maisha yake." Anaeleza. "Sasa tunataka watu wasikie kile ambacho raia wa Syria walikipitia."
Abdullah, 36, alikuwa anafanya kazi mjini Damascus kama muuza duka na kamati ya msalaba mwekundu mwezi Julai mwaka 2013 pale yeye na wafanyakazi wenzake waliposimamisha katika eneo la ukaguzi nje kidogo ya mji mkuu wa Syria.
Alisema alishiriki kwenye maandamano ya kupinga utawala uliopita mwaka 2011 katika mji wa kusini wa Deraa, eneo ambalo upinzani dhidi ya Assad ulipoanzia, lakini punde tu baada ya hapo alijitoa baada ya waasi kuanza kutumia ghasia na silaha wakijibu mashambulizi yaliyokuwa yakifanywa na vikosi vya serikali iliyokuwa madarakani.

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika eneo la ukaguzi, Abdullah aliwekwa kando na kupandishwa kwenye basi la kijani, akiwa amefungwa pingu mikononi na kuzibwa macho, na kupelekwa katika eneo la jeshi. Anasema baada yah apo aliwekwa kwenye chumba cha peke yake kwa siku tatu ambapo pia alipigwa.
"Nakumbuka kulikuwa na giza sana kwa siku tatu," anasema.
"Nilikuwa sisikii sauti yoyote. Kulikwa na giza sana. Husikii chochote. Unajihisi mpweke sana."
Kisha Abdullah alisafirishwa na kupelekwa kwenye gereza la Al-Khatib, lililopo mjini Damascus na kupelekwa kwenye chumba chenye takriban watu 130.
Al-Khatib lilikuwa moja ya magereza kadhaa yanayoendeshwa na mamlaka za kijasusi za Syria.
Kulingana na shirika la uchunguzi la masuala ya haki za kibinadamu Syria lililopo nchini Uingereza, Takriban watu 60,000 waliteswa na kuuawa ndani ya magereza yaliyoendeshwa na uongozi wa Assad wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Miaka miwili iliyopita, mashtaka yaliyokuwa yakisikilizwa nchini Ujerumani yalimkuta kanali aliyefanya kazi ndani ya Al-Khatib na hatia kwa uhalifu kinyume na ubinadamu. Anwa Raslan, 58, alihusishwa na uteswaji wa zaidi ya watu 4,000 ndani ya gereza hilo.
Ndani ya mahakama, mashahidi walielezea jinsi wafungwa walivyo bakwa na kuning'iniza kutoka kwenye paa kwa saa nyingi, pamoja na watu kupigwa na shoti za umeme kabla ya kuingizwa kwenye maji. Huko nyuma, Serikali ya utawala wa mabavu wa Assad ilikataa shutuma za kuwatesa watu.
'Kila dakika ni kama una kufa'
Wakati anashikiliwa mwaka 2013, Abdullah ameelezea jinsi alivyokuwa anasikiwa kelele za watu wakati wakiteswa.
Anakumbuka jinsi gani magonjwa yalienea na karibu watu ishirini walikufa wakati anashikiliwa katika gereza hilo.
"Nilipoanza kuangalia mazingira yangu yaliyokuwa yananizunguka, niliona watu wamesimama wakiwa nusu uchi," anaiambia BBC. "Walikuwa wanatokwa damu, kama vile wametoka kuteswa."
"Kama wewe mwenye haukuteswa, kila dakika walikuwa wanapeleka mtu mmoka kwenye chumba cha uchunguzi."
Wakirudi wanakuwa wamelowa damu…pale unapojaribu kumgusa mtu basi watapiga kelele kwasababu unakuwa umegusa kidonda fulani"
Baada ya siku 12, Abdullah alichukuliwa kwenda kuulizwa maswali, ambapo anasema alipigwa mara kadhaa na silaha ya chuma na kutuhumiwa kwa makosa ya usafirishaji wa silaha.
Anaeleza jinsi gani alishindwa kukataa mashtaka dhidi yake kwasababu ingemfanya aendelee kuadhibiwa.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ikiwa utakanusha mashtaka dhidi yako, na kusema 'sikufanya hivyo' basi wataendelea kukutesa na watakupeleka kwenye hatua nyingine ya kuteswa," anasema.
"Kila dakika ni kama unakufa."
Abdullah alisema aliwaambia maafia uongo ili asiendelee kuulizwa maswali na alikuwa na "bahati" kuachiliwa huru baada ya mwezi mmoja.
Miaka kadhaa baadaye, aliondoka nchini Syria na kupewa ufadhili mjini Geneva na Marekani. Kwasasa anaishi London na mke wake.
Ni sasa tu ndipo Abdullah ameweza kumuelezea mke wake yale aliyoyapitia, kwasababu hali ya hatari na hofu aliyokumbana nayo inaanza kupotea kidogo kidogo.
"Hatimaye tumemalizana na utawala wa Assad, tunaweza kusema, tupo huru sasa," anasema
"Unaweza kutumia jina letu. Unaweza kutumia sura zetu. Tunaweza kusema yale tuliyoyapitia."
Douna ni mwanaharakati wa kutetea haki za kibinadamu, alilia wakati akisikia yale aliyopitia mume wake kwa mara ya kwanza.
"Nilikuwa namsikiliza na nilikuwa nalia. Utawala uliopita umefanya maovu makubwa yasioelezeka." Anasema.
"Inanishangaza sana kuwa, hayo ni mambo kadhaa tu yaliyokuwa yakiendelea. Kuna uwezekano wa kuwepo kwa mengine zaidi."
Douna anasema "Tuna bahati sana kuwa tunaweza kusimulia yale tuliyoyapitia. Watu wengi, walikufa bila kusikika."