Makubaliano ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China ya kutekeleza mpango wa kistratejia wa nchi mbili
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China wametathimini kuwa chanya mchakato unaopiga hatua wa kutekeleza vipengee vya ushirikiano wa kistratejia katika miaka ya karibuni.
Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye yuko ziarani nchini China akiongoza ujumbe rasmi wa ngazi amekutana na kufanya mazungumzo na Wang Yi, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo. Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran China wamesisitiza katika mazungumzo hayo kuwa watafanya juhudi kutekeleza mpango wa ushirikiano wa kina kati ya nchi mbili katika kivuli cha miongozo ya kimkakati ya viongozi wa nchi mbili na kuimarisha mabadilishano ya tajiriba za kiuongozi na kiutendaji katika nyanja za kisiasa, kidiplomasia, kibunge, kiulinzi, kiusalama, kijeshi, masuala ya anga, uchumi na biashara.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi mbili pia wamesisitiza udharura wa kuimarisa ushirikiano katika nyanja za vijana, elimu, michezo, sayansi na teknolojia, utamaduni, utalii, mazingira, afya na tiba, redio na televisheni.
Araqchi ameandika katika mtandao wa kijami wa X kwamba amekuwa na majadiliano muhimu na ya kina na mwenzake wa China, Wang Yi, kuhusu masuala mbalimbali yanayozihusu pande mbili, kikanda na kimataifa.
Iran na China zikiwa nchi washirika wa kimkakati zimeazimia kupanua mashauriano ili kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kukuza maslahi ya mataifa hayo, na vilevile kutoa mchango wa kuboresha utawala wa sheria na kukuza amani na usalama kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na China pia wamejadili umuhimu wa kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na ugaidi, kuimarisha utawala wa sheria katika ngazi ya kimataifa, suala la nyuklia na kuondoa vikwazo na pia kupanua ushirikiano katika fremu ya taasisi ambazo pande zote mbili ni nchi wanachama ikiwa ni pamoja na kundi la BRICS na Jumuiya ya Shanghai. Araqchi pia amesema Iran inaunga mkono China kuwa mwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai katika mwaka ujao wa 2025.
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na China wametia saini hati ya mpango wa pamoja wa ushirikiano au mpango wa miaka 25 uliotayarishwa mjini Tehran Machi 27 mwaka 2021. Katika miaka ya karibuni, Maafisa wa ngazi za juu wa Iran na China wamekuwa wakitilia mkazo utekelezaji wa hati hiyo ya ushirikiano. Iran na China zimekubaliana kutekeleza mpango wa pamoja wa ushirikiano kama ramani ya njia ili kufikiwa ushirikiano wa kistratejia baina ya pande mbili.

Viongozi wa Tehran na Beijing wanatilia mkazo kwamba hati hii ya ushirikiano inapaswa kutambuliwa na kuzingatiwa kuwa mpango wa kimkakati wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni katika nyanja tofauti za kisiasa, kistratejia, kiuchumi na kiuchumi na kiutamaduni kwa muda mrefu.
Moja ya vipengele muhimu vya hati hiyo ni namna ulivyojikita katika masuala ya uchumi na unavyotoa kipaumbele katika suala la kuimarisha uhusiano wa nchi mbili katika nyanja mbalimbali za kibiashara na kiuchumi. Iran na China zinasisitiza kuwa uwezo wa ushirikiano wa kiuchumi kati yao ni mkubwa; na kwa mukhtadha huu nchi mbili zinasisitiza kuimarisha ushirikiano katika nyuga za mafuta, viwanda na madini na katika nyanja nyingine zinazohusiana na nishati ikiwemo nishati jadidika.