Ndege za kivita za Ufaransa zaondoka Chad
Ndege za kivita za Ufaransa zaondoka Chad
Ndege mbili aina ya Mirage 2000D zilizoambatana na ndege ya kujaza mafuta zilizoko Chad zimepaa siku ya Jumanne kutoka N'Djamena, na kuzindua zoezi la kuondoka kwa jeshi la Ufaransa nchini Chad baada ya kusitishwa kwa makubaliano ya ulinzi na Chad. Ndege ya tatu ilikuwa imepangwa kupaa wakati wa mchana.
"Kuwepo kwa kikosi hiki sio haki tena baada ya kuvunjika kwa makubaliano ya ulinzi", yaliyoshtumiwa Novemba 28 na mamlaka ya Chad, kulingana na chanzo kingine cha Ufaransa. "Ufaransa inafunga kikosi cha ndege za kivita katika kituo cha anga cha Kossei huko N'Djamena. Jeshi la Ufaransa linachukua uamuzi wa kuondoa ndege zake," chanzo hiki kimeongeza.
Chad ilikuwa kiungo muhimu katika uwepo wa jeshi la Ufaransa barani Afrika, ikijumuisha kituo cha mwisho cha Paris katika Sahel baada ya kulazimishwa kuondoka kwa wanajeshi wake huko Mali, Burkina Faso na Niger. Kuondoka kwa ndege hizi aina ya Mirages ni matokeo ya tangazo la Chad, katika kumbukumbu ya uhuru wake mnamo Novemba 28, kumaliza makubaliano ya usalama na ulinzi ambayo yaliunganisha nchi hizo mbili.
Hadi wakati huo, Paris iliweka karibu wanajeshi 1,000 nchini Chad kwenye kambi kadhaa za kijeshi, mfumo ambao ulipaswa kupunguzwa kama sehemu ya urekebishaji wa uwepo wa jeshi la Ufaransa huko Senegal, Côte d'Ivoire na Chad ambapo mjumbe binafsi wa Emmanuel Macron barani Afrika, Jean-Marie Bockel, alikuwa na jukumu la kushauriana na nchi mbalimbali.
Ndege za kivita za Ufaransa zimekuwa zikipiga kambi nchini Chad, takriban mara kwa mara tangu uhuru mwaka 1960, zikifanya kazi kwa mafunzo na mazoezi ya wanajeshi wa Chad lakini pia kwa usaidizi wa anga, na hivyo kufanya iwezekane mara kadhaa kusimamisha harakati za waasi kutaka kunyakua madaraka.