Rais anayeondoka wa Georgia akataa kujiuzulu huku mrithi wake akiapishwa

Chanzo cha picha, Reuters/EPA
Maelfu ya wananchi wa Georgia wameandamana katika mji mkuu wa Tbilisi huku rais mpya wa chama tawala cha Georgian Dream party akiapishwa.
Mikheil Kavelashvili, mchezaji soka wa zamani, ameapishwa katika kipindi kigumu cha kisiasa nchini humo baada ya serikali kusitisha ombi lake la kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Georgian Dream kilishinda uchaguzi wa bunge mwezi Oktoba, lakini ushindi huo uligubikwa na madai ya udanganyifu ambayo tangu wakati huo yamesababisha maandamano mitaani.
Rais anayemaliza muda wake Salome Zourabichvili alikataa kujiuzulu siku ya Jumapili, akisema ndiye "rais pekee halali".
Akihutubia umati uliokusanyika nje, Zourabichvili alisema ataondoka ikulu ya rais lakini akamtaja mrithi wake kuwa haramu.