Rais wa Kenya aahidi kukomesha utekanyaji nyara ili vijana wa nchi hiyo waishi kwa amani


  • Rais wa Kenya aahidi kukomesha utekanyaji nyara ili vijana wa nchi hiyo waishi kwa amani

Rais William Ruto wa Kenya ameahidi kukomesha utekaji nyara, kufuatia visa vya hivi karibuni vya watu kutoweka ambavyo vimelaaniwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu, mawakili na wanasiasa.

Vikosi vya usalama katika taifa hilo la Afrika Mashariki vimeshutumiwa kwa kuwashikilia watu kadhaa kinyume cha sheria tangu yalipofanyika maandamano yaliyoongozwa na vijana dhidi ya serikali katika miezi ya Juni na Julai.

Polisi wamekanusha kuhusika lakini wanaharakati wamehoji ni kwa nini wanaonekana kutochunguza kupotea kwa watu hao.

Utowekaji wa hivi karibuni wa watu umehusisha hasa vijana ambao wamemkashifu Ruto mtandaoni, huku mashirika ya kutetea haki ya binadamu yakikanusha madai ya polisi kutohusika na kutaka hatua zichukuliwe.

Akizungumza na umati wa watu jana Ijumaa huko Homa Bay, mji ulioko magharibi mwa Kenya, Rais Ruto aliahidi kukomesha utekaji nyara huo lakini pia akawaambia wazazi "kuwajibikia" watoto wao.

"Tutakomesha utekaji nyara ili vijana wetu waishi kwa amani," alisema kiongozi huyo. 

Wimbi la hasira limeendelea kuongezeka nchini Kenya, huku matukio ya hivi punde ya utekaji nyara yakizusha maandamano madogo katika angalau mji mmoja.

"Ikiwa kweli polisi hawajahusika," Chama cha Wanasheria cha Kenya kilisema, lazima "wachunguze na kuwashtaki waliohusika" mara moja.

Matamshi ya Ruto yanafuatia maoni ya hivi majuzi ya aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua, ambaye alidai kitengo cha siri ndicho kilihusika na kutoweka kwa watu hao.../