Senegal kufunga vituo vyote vya kijeshi vya kigeni, ni vilivyosalia vya Ufaransa vilivyoko nchini humo
Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane Sonko amesema, nchi hiyo itafunga kambi zote za kijeshi za kigeni katika ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kupitia upya sera ya ulinzi na kuimarisha mamlaka ya kitaifa.
Sonko alitangaza uamuzi huo katika Bunge la Taifa hapo jana
wakati wa uwasilishaji sera kuu, ambapo alielezea mkakati wa mabadiliko
ya taifa hilo la Afrika Magharibi katika miaka 25 ijayo.
"Rais wa Jamhuri ameamua kufunga kambi zote za kijeshi za kigeni katika siku za usoni," Sonko alisema.
Waziri Mkuu wa Senegal hakutaja nchi maalumu, lakini Ufaransa ndiyo nchi pekee ya kigeni yenye wanajeshi nchini humo.
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, ambaye amekuwa madarakani
kwa muda wa chini ya mwaka mmoja, alitangaza kwa mara ya kwanza uamuzi
wake wa kuondoa jeshi la Ufaransa nchini mwake katika mahojiano na
shirika la habari la AFP mwishoni mwa mwezi uliopita. Alisema kambi za
jeshi la Ufaransa "hazikidhi" kulindwa mamlaka ya kujitawala ya nchi
hiyo ya Afrika Magharibi.
Kwa sasa Ufaransa ina wanajeshi 350 nchini Senegal.
Ufaransa imekumbwa na misukosuko katika makoloni yake kadhaa ya
zamani barani Afrika huku kukiwa na wimbi la chuki dhidi ya nchi
hiyo lililochochewa na kushindwa kukabiliana na uasi wa wanamgambo, na
shutuma za kuingilia masuala ya ndani ya nchi hizo na kufanya uchokozi.
Dola hilo la kikoloni la zamani lilikuwa na zaidi ya wanajeshi
5,000 katika eneo la Sahel kama sehemu ya Operesheni Barkhane,
iliyohudumu kwa muongo mmoja katika kampeni ya kijeshi ya kukabiliana na
waasi ambayo ilimalizika mwishoni mwa 2022 wakati Paris ilipoondoa
jeshi lake nchini Mali kutokana na kuvunjika uhusiano kufuatia mapinduzi
ya Bamako Mei 2021.../