Syria: Kiongozi mpya akutana na wawakilishi wa serikali ya magharibi mwa Libya

 Kiongozi huyo mpya wa Syria amekutana Jumamosi na maafisa wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, ujumbe wa hivi punde zaidi wa kidiplomasia kuzuru Damascus tangu kuondolewa madarakani kwa Bashar Al Assad karibu wiki tatu zilizopita.

Kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Kiislamu nchini Syria Hayat Tahrir al-Sham (HTS) aliyeongoza mashambulizi makubwa na kunyakua Damascus kutoka kwa udhibiti wa serikali, Abu Mohammed al-Jolani, akiwasili ndani ya Msikiti wa Umayyad katika mji mkuu wa Syria kuhutubia umati uliokusanyika hapo tarehe 8 Disemba. 2024. Jolani, sasa anatumia jina lake halisi Ahmed al-Sharaa, alitoa hotuba huku umati ukimsifu Mungu "Allahu akbar (Mungu ni mkuu)," video iliyoshirikiwa na waasi kwenye chaneli yao ya Telegram.
Kiongozi wa kundi la wapiganaji wa Kiislamu nchini Syria Hayat Tahrir al-Sham (HTS) aliyeongoza mashambulizi makubwa na kunyakua Damascus kutoka kwa udhibiti wa serikali, Abu Mohammed al-Jolani, akiwasili ndani ya Msikiti wa Umayyad katika mji mkuu wa Syria kuhutubia umati uliokusanyika hapo tarehe 8 Disemba. 2024. Jolani, sasa anatumia jina lake halisi Ahmed al-Sharaa, alitoa hotuba huku umati ukimsifu Mungu "Allahu akbar (Mungu ni mkuu)," video iliyoshirikiwa na waasi kwenye chaneli yao ya Telegram. AFP - AREF TAMMAWI
Matangazo ya kibiashara

"Tunatoa uungwaji mkono wetu kamili kwa mamlaka ya Syria katika awamu hii muhimu ya mpito," Waziri wa Nchi wa Libya anayehusika na Mawasiliano Walid Ellafi amewaambia waandishi wa habari, baada ya mkutano wake na Ahmad al-Shareh, kiongozi wa kundi la Kiislamu linalotawala muungano uliompindua Assad. 

Amesisitiza juu ya "umuhimu wa ushirikiano wa pamoja", katika nyanja za usalama, kijeshi na nishati, na pia katika suala la "uhamiaji haramu" ambao unaathiri nchi zote mbili, kulingana na Walid Ellafi.

Katika kukabiliwa na machafuko tangu kuanguka na kifo cha dikteta Muammar Gaddafi mwaka 2011, Libya inatawaliwa na serikalii mbili hasimu, ile ya Abdelhamid Dbeibah iliyeko Tripoli (magharibi) na inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, na ile inayoshirikiana na Marshal Khalifa Haftar, nchini humo mashariki mwa nchi.

Libya ilifunga uwakilishi wake huko Damascus mnamo mwaka 2012 lakini mnamo Machi 2020, wawakilishi wa Marshal Haftar walifungua tena ujumbe wa kidiplomasia huko Damascus na bendera ya Libya ilipandishwa.

Haijulikani kama wanadiplomasia hawa wa Libya waliotumwa na mamlaka ya mashariki bado wako Syria tangu kuanguka kwa Bashar Al Assad na kutekwa kwa Damascus tarehe 8 Desemba na muungano wa makundi yenye silaha yanayoongozwa na Waislam wa Hayat Tahrir al-Sham. (HTS).

Bw. Ellafi pia ametoa wito wa "kuimarishwa" kwa uhusiano wa kidiplomasia, akisema angependa kuwasili kwa "balozi wa kudumu huko Damascus" ambako kwa sasa kuna tu maafisa wa Libya.

Siku ya Jumamosi pia, picha zilizorushwa na shirika la habari serikali ya Syria SANA zimeonyesha mkutano kati ya kiongozi mpya wa Syria na mkuu wa ofisi ya mikakati ya usalama ya Bahrain, Sheikh Ahmad bin Abdulaziz al-Khalifa.

Wakati wa ziara hii, wawili wamejadili "umuhimu wa kulinda usalama wa kikanda" na uungaji mkono wa Manama kwa "mchakato shirikishi wa mpito unaopendelea maridhiano, ufufuaji wa uchumi na misaada ya kibinadamu kwa watu wa Syria", msemaji wa serikali ya Bahrain ameliambia shirika la habari la AFP.

Siku chache baada ya kuangushwa kwa Assad, Mfalme wa Bahrain, Hamad bin Issa Al Khalifa, alisema yuko tayari kushirikiana na mamlaka mpya nchini Syria katika barua aliyoituma kwa Ahmad al-Shareh.

Uturuki, ambayo inaunga mkono mamlaka mpya ya Syria na utawala wa Tripoli magharibi mwa Libya, ilimtuma Waziri wake wa Mambo ya Nje kwenda Damascus siku ya Jumapili.

Hakan Fidan alikuwa ametaka vikwazo dhidi ya Syria viondolewe "haraka iwezekanavyo" na kwa jumuiya ya kimataifa "kuhamasishwa kusaidia Syria kurejea katika nyayo zake."

Tangu tarehe 8 Desemba, wajumbe wengi kutoka nchi za Kiarabu na Magharibi wameendelea kuja Damascus.