Trump aitaka Mahakama ya Juu ya Marekani kuchelewesha marufuku ya TikTok

 

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Rais mteule wa Marekani Donald Trump

Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameiomba Mahakama ya Juu ya Marekani kuchelewesha marufuku inayokuja ya TikTok huku akifanyia kazi "azimio la kisiasa".

Wakili wake aliwasilisha muhtasari wa kisheria siku ya Ijumaa na mahakama ambayo inasema Trump "anapinga kupigwa marufuku kwa TikTok" na "anatafuta uwezo wa kutatua masuala yaliyopo kupitia njia za kisiasa mara tu atakapoingia madarakani".

Tarehe 10 Januari, mahakama inatazamiwa kusikiliza hoja kuhusu sheria ya Marekani inayomtaka mmiliki wa TikTok Mchina, ByteDance, kuiuza kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kwa kampuni ya Kimarekani la sivyo apigwe marufuku ifikapo Januari 19 - siku moja kabla ya Trump kuchukua madaraka.

Maafisa wa Marekani na wabunge walikuwa wameshutumu ByteDance kwa kuhusishwa na serikali ya China - jambo ambalo kampuni hiyo inakanusha.

Madai hayo ya programu ambayo ina watumiaji milioni 170 nchini Marekani yalisababisha Bunge la Congress kupitisha mswada mwezi Aprili, ambao Rais Joe Biden alitia saini kuwa sheria, ambayo ni pamoja na sharti la kupiga marufuku.

TikTok na ByteDance wamewasilisha changamoto nyingi za kisheria dhidi ya sheria hiyo, wakisema kwamba inatishia ulinzi wa uhuru wa kujieleza wa Marekani,

Kwa kuwa hakuna mnunuzi aliyepatikana kufikia sasa, nafasi ya mwisho ya kampuni hiyo kukomesha marufuku hiyo imekuwa kupitia mahakama kuu ya Marekani.

Ingawa Mahakama ya Juu hapo awali ilikataa kufanyia kazi ombi la zuio la dharura dhidi ya sheria, ilikubali kuruhusu TikTok, ByteDance na serikali ya Marekani kusihi kesi zao tarehe 10 Januari - siku chache kabla ya marufuku hiyo kuanza kutekelezwa.