Ipi tofauti kati ya mashambulizi ya 1991 ya Iraq na 2024 ya Iran dhidi ya Israel?

 


shambulio la Iran, usiku wa Jumamosi iliyopita la ndege zisizo na rubani na makombora lilikuwa la kwanza la aina yake dhidi ya Israel tangu mashambulizi ya makombora yaliyoanzishwa na Iraq wakati wa Vita vya Pili vya Ghuba zaidi ya miongo mitatu iliyopita.

Januari 17, 1991, Vita vya Pili vya Ghuba vilianza, wakati vikosi vya muungano wa kimataifa vinavyoongozwa na Marekani vilipofanya operesheni ya kijeshi ya anga na ardhini dhidi ya Iraq kujibu uvamizi wake wa Kuwait wa Agosti 1990.

Januari 18, 1991, yaani, siku moja tu baada ya kuzuka kwa vita hivyo, rais wa wakati huo wa Iraq, Saddam Hussein, alianza kuishambulia Israel kwa takribani makombora 40 ya Scud.

Ni jaribio ambalo waangalizi wanaamini lilikuwa na lengo la kuiingiza Israel katika mzozo huo ili kuleta mpasuko katika kambi ya nchi za Kiarabu na Kiislamu zilizolaani kuvamiwa Kuwait.

Makombora hayo yalishambulia Tel Aviv, Bandari ya Haifa, na Jangwa la Negev, ambapo kinu cha nyuklia cha Dimona kinapatikana.

Mashambulizi ya Iran

tygf

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Raia wa Israel wakiwa katika ufukwe wa Tel Aviv siku moja baada ya mashambulio ya Iran

Ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus ulikumbwa na shambulizi la anga mwanzoni mwa mwezi huu na kusababisha vifo vya watu 13 wakiwemo makamanda wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, wakiongozwa na kamanda wa Kikosi cha Quds Mohammad Reza Zahedi.

Israel haijathibitisha kuwa ilifanya shambulizi hilo, lakini inaaminika kuwa ilifanya. Iran ililichukulia shambulizi hilo la anga kama shambulio la wazi la Israel dhidi yake, na ikaapa kujibu.

Jibu hilo lilikuja Aprili 13, wakati makombora ya balestiki, roketi na droni zilirushwa kwenda Israel. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Iran kuishambulia Israel moja kwa moja, mpinzani wake wa kikanda.

Nchi hizo mbili zimekuwa zikiendesha kile ambacho wataalamu wanakiita vita vya chini chini kwa miaka, kwani kila moja huwa inashambulia shabaha za nchi nyingine bila kukiri kuhusika.

Kamanda Mkuu wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran, Hossein Salami, alisema operesheni hiyo, ambayo Iran iliiita Ahadi ya Kweli, ililenga kituo cha kijasusi cha Israel kaskazini mwa Golan na kambi ya Nevatim, inayohifadhi ndege za kivita za F 35 katika Jangwa la Negev kusini mwa Israel.

Maafisa wa Israel walisema ni makombora machache ya balistiki ndio yalisababisha uharibifu mdogo kwenye kituo cha Nevatim, lakini kituo hicho bado kinafanya kazi, kama msemaji wa jeshi la Israel Daniel Hagari alivyoeleza.

FD

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mwanajeshi wa Israel akimsaidia mzee mmoja kuvaa barakoa ya gesi - akitarajia nchi hiyo kushambuliwa kwa silaha za kemikali na Iraq mwaka 1991.

Mashambuliz hayo yalimjeruhi msichana wa miaka 7 kutoka kijiji cha Bedouin katika eneo la Negev, kulingana na vyombo vya habari vya Israel. Hakukuwa na taarifa za kupoteza maisha.

Israel ilisema iliweza kuzuia asilimia 99 ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran. Kwa usaidizi wa washirika wa Israel, wakiongozwa na Marekani.

Jordan pia ilisema ilinasa vitu vinavyoruka vilivyoingia katika anga yake ili kuhakikisha usalama wa raia wake, na jeshi la Israeli lilisema Ufaransa ilisaidia kulinda anga, lakini haijabainika ikiwa ilitungua kombora lolote la Iran au ndege zisizo na rubani.

Mashambulizi ya Iraq

FGV

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Mwanaume wa Israel alinasa chini ya vifusi vya nyumba yake, ambayo ilipigwa na kombora la Iraq Februari 12, 1991.

Mwaka 2021, katika hafla ya kuadhimisha miaka thelathini ya shambulio la makombora la Iraq dhidi ya Israel, jeshi la Israel liliruhusu kuchapishwa sehemu ya kumbukumbu zake, ambayo ilifichua kwamba mashambulizi hayo ya Januari 18 na Februari 25, 1991, yalisababisha vifo 14 na majeruhi zaidi ya 200 ya moja kwa moja.

Na wengine zaidi ya 500 walitibiwa kutokana na hofu na mshituko, na zaidi ya watu 200 ambao walijidunga dawa ya atropine bila ushauri wa daktari.

Video za kumbukumbu zilizochapishwa na vyombo vya habari vya Israel zinaonyesha - majengo yalivyoharibiwa na viwanda vingine vikiwaka moto.

Vikosi vya uokoaji vilichukulia makombora yoyote ya Iraq kama kemikali, na kwa hivyo walivaa mavazi ya kujikinga walipoelekea maeneo ambayo makombora haya yalianguka.

Baada ya mashambulizi ya Iran

REF

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Ndege isiyo na rubani aina ya Shahed-136 iliyotengenezwa na Iran. Iran ilirusha makumi ya ndege zisizo na rubani na makombora kwenda Israel usiku wa Jumamosi iliyopita

Marekani ilitoa shinikizo kubwa la kidiplomasia kwa Israel isifanye mashambulizi ya kulipiza ya moja kwa moja dhidi ya Iran.

Israel ilikubali kutojibu, lakini kwa upande wake iliitaka Washington kupeleka mara moja mifumo ya ulinzi ya makombora ya Patriot ya kupambana na makombora ya balestiki.

Rais wa Marekani Joe Biden amerejelea ahadi ya nchi yake katika kulinda usalama wa Israel, lakini afisa wa ngazi wa serikali ya Marekani alisema nchi hiyo haitashiriki katika mashambulizi yoyote ya kulipiza kisasi yatakayo anzishwa na Israel dhidi ya Iran.

Biden alimtumia Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ujumbe wa wazi akisema: "Shambulio la Iran limezuiwa, na Israel imeshinda, hivyo usizidishe mgogoro kwa kujibu mashambulizi ya kijeshi katika ardhi ya Iran."

Kwa upande wa Israel, ilitangaza itajibu shambulio la Iran "kwa jinsi itakavyochagua na kwa wakati ipendayo."

Wakati hali ya wasiwasi imetanda Mashariki ya Kati ya vita kupanuka tangu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7 dhidi ya Israel na uvamizi wa Gaza. Inahofiwa kuwa hatua yoyote ya serikali ya Israel, kuishambulia Iran itasababisha mgogoro huo kupanuka.

 

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China