Kwa nini Israel inafanya mashambulizi ya fosforasi nyeupe huko Gaza na Lebanon?

 

Picha hii ilipigwa Oktoba 16 katika kijiji cha Dhahira kusini mwa Lebanon, ikionesha moshi wenye umbo la pweza ukiendelea kupaa, huku maganda yenye sumu yakianguka chini.

Chanzo cha picha, AP

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Israel imeendelea kutumia mabomu ya fosforasi nyeupe kuvuka mpaka wa kusini mwa Lebanon. Ikiwa ni gesi yenye sumu, inadhuru macho na mapafu na inaweza kusababisha hali ya kuchoma, na kwa hivyo matumizi yake yanadhibitiwa chini ya sheria za kimataifa.

Jeshi la Israel linasema kuwa matumizi yake ya silaha hii yenye utata dhidi ya wanamgambo wa Gaza na Lebanon ni halali. Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema suala hilo linafaa kuchunguzwa kama uhalifu wa kivita.

Wamarekani wanasema watachunguza matumizi ya Israel ya fosforasi nyeupe katika nchi zote mbili.

Je, kwa kutumia silaha karibu na raia, majeshi ya Israel yanakiuka sheria? Au hii inazingatiwa kweli wakati wa vita?

"Silaha hii inaruka kama ukungu mweupe. Lakini inapofika ardhini, inageuka kuwa unga.

Ali Ahmed Abu Samra, mkulima mwenye umri wa miaka 48 kutoka kusini mwa Lebanon, anasema alijikuta akizungukwa na wingu zito la moshi mweupe mnamo Oktoba 19, 2023.

"Wanasema ina harufu ya kitunguu saumu, lakini ni mbaya zaidi. Harufu ilikuwa isiyovumilika. Mbaya zaidi kuliko maji taka,” ndivyo Ali alielezea shambulio la fosforasi nyeupe

Ali Ahmed Abu Samra

Mabomu ya fosforasi nyeupe huwaka kwa joto la hadi nyuzi joto 815, na yanaweza kushika moto na pia yana sumu kali.

Ali, kutoka kijiji cha Dhahira, anasema, "Maji yalianza kutiririka kutoka machoni mwetu... Kama tusingekuwa tumeziba midomo na pua zetu kwa vitambaa vyenye unyevunyevu, tusingekuwa hai leo."

BBC ilithibitisha matumizi ya mara kwa mara ya silaha ya fosforasi nyeupe na jeshi la Israeli, katika miji na vijiji vinne nchini Lebanon kati ya Oktoba 2023 na Machi 2024.

Tangu kuanza kwa vita huko Gaza mwezi Oktoba mwaka jana, ghasia pia zimeongezeka katika mpaka wa Israel na Lebanon, na kusababisha hasara kwa pande zote mbili na maelfu ya watu kuyahama makazi yao.

Hezbollah, inayoshirikiana kwa karibu na Iran na mshirika wa Hamas, inachukuliwa kuwa moja ya vikosi vya kijeshi visivyo vya kiserikali vilivyo na silaha nyingi zaidi ulimwenguni.

Mashambulizi ya roketi na ndege zisizo na rubani, yanayoanzishwa na wapiganaji wa Hezbollah karibu kila siku, yamekabiliwa na mashambulizi makubwa ya anga na mizinga ya jeshi la Israel, ikiwa ni pamoja na matumizi ya fosforasi nyeupe.

Fosforasi nyeupe imetumiwa na vikosi vingi vya ulimwengu katika karne iliyopita. Ilitumiwa sana na Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, kulingana na CIA.

Marekani pia ilikubali matumizi yake nchini Iraq mwaka 2004, na kisha tena nchini Syria na Iraq dhidi ya ISIS mwaka 2017.

Israel pia iliripoti kutumia kemikali hii wakati wa shambulio la 2008-2009 huko Gaza. Lakini baada ya Umoja wa Mataifa kusema jeshi la Israel "lilipuuza kimfumo" katika suala hili, jeshi la Israeli lilisema mnamo 2013 kwamba "silaha hii itaondolewa katika utumishi wa kijeshi hivi karibuni."

Inajulikana kuwa wapiganaji wa Hezbollah wanahamia katika vitengo vidogo, vinavyojumuisha watu wawili hadi wanne. Wanatumia vichaka kwa ajili ya kujifunika, na mara nyingi kurusha makombora na makombora kuvuka mpaka kuelekea jeshi la Israeli lililoko upande mwingine. Kuwafurika kwa moshi inaweza kuwa mojawapo ya njia zinazotumiwa na Waisraeli.

Katika siku ambazo kijiji cha Ali (Dhahira) kilishambuliwa kuanzia Oktoba 10 hadi 19, Ali alisema hakukuwa na makundi yenye silaha katika eneo hilo.

"Kama Hezbollah ingalikuwapo, watu wangewataka kuondoka kwa sababu hawakutaka kufa," Ali anasema. "Hezbollah haikuwepo."

BBC haikuweza kuthibitisha kuwepo au kutokuwepo kwa makundi yoyote yenye silaha katika kijiji hicho katika siku yalipofanyika mashambulizi hayo.

BBC ilithibitisha kwa uhuru mashambulizi zaidi katika kijiji cha Marjayoun, Machi 4, 2024

Chanzo cha picha, Reuters

Wa kwanza kufika eneo la tukio mchana alikuwa ni mtu wa gari la wagonjwa la kujitolea, Khaled Quraitem.

"Tulianza kuwaondoa watu ambao walipoteza fahamu," Khaled anasema. Lakini walipokuwa bado wanajaribu kuwafikia watu, timu ya uokoaji ilishambuliwa.

"Waliturushia makombora matatu," Khaled anasema. "Ama kutuzuia kuokoa watu au kutengenezavmazingira ya hofu."

Khaled anakumbuka kuwasafirisha takribani watu tisa hadi hospitali ya Italia huko Tyre, akiwemo baba yake, Ibrahim.

Ibrahim, mwenye umri wa miaka 65, alilazwa hospitalini kwa siku tatu kutokana na matatizo makubwa ya kupumua. Daktari wake, Dk. Muhammad Mustafa, anasema amewatibu wagonjwa wengi waliokuwa wameathiriwa na fosforasi nyeupe.

BBC ilithibitisha shambulio la fosforasi nyeupe kwenye kijiji cha Aita al-Shaab mnamo Oktoba 15.

Chanzo cha picha, AP

Tulipokwenda kukutana na Ibrahim miezi mitatu baadaye, macho yake bado yalikuwa mekundu, na ngozi ya mikono na miguu yake ilikuwa na vipele na magamba. Anasema kwamba madaktari walimwambia kuwa sababu ya yote haya ni fosforasi nyeupe.

"Tangu miaka ya 1970, tumekuwa tukiishi katika vita," Ibrahim anasema. "Lakini hakuna kitu kama hiki, hakijawahi kutokea. Milipuko hutokea karibu na nyumba zetu.”

Aliongeza kuwa ganda moja lilianguka mita sita kutoka kwenye gari lake, alipokuwa akijaribu kutoroka. Anasema kulikuwa na ndege zisizo na rubani za jeshi la Israel zikiruka angani.

"Wangeweza kutuona," Ibrahim anasema. "Walikuwa wakipiga risasi bila mpangilio."

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema kwamba shambulio la kijiji cha Dhahira "linapaswa kuchunguzwa kama uhalifu wa kivita, kwa sababu lilikuwa ni shambulio la kiholela ambalo lilijeruhi takribani raia tisa, na kusababisha athari kwa raia, hivyo halikuwa halali.

Ushahidi wa fosforasi nyeupe

Mara tu baada ya shambulio la kijiji cha Ali (mchana), ripoti zilianza kuonekana mtandaoni. Hapo awali, jeshi la Israeli lilikana kutumia mabomu ya fosforasi nyeupe, lakini baadaye lilighairi na kukubali matumizi yake, lakini "ndani ya sheria za kimataifa."

Kwa kuchunguza ushahidi wote uliopo, BBC iliweza kuthibitisha matumizi ya fosforasi nyeupe saa sita mchana, pamoja na vijiji vingine vitatu kwenye mpaka katika kipindi cha miezi sita iliyopita.

BBC ilithibitisha shambulio la fosforasi nyeupe kwenye kijiji cha Kafr Kila, kinachokaliwa na watu wapatao 14,000, mnamo Novemba 22, 2023.

Chanzo cha picha, AP

Katika kijiji cha Kafr Kila, BBC ilipata kipande cha ganda kilichoanguka kati ya nyumba mbili za raia, na kukifanyia uchunguzi wa kemikali. Uchunguzi huo ulifanywa na profesa maarufu wa kemia. Kwa sababu za kiusalama, aliomba utambulisho wake usifichuliwe.

 Profesa wa Kemia anaonesha ishara kwamba ganda hilo limetengenezwa Marekani. Mapema mwaka huu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema itachunguza matumizi haramu ya mabomu nyeupe ya fosforasi yaliyotengenezwa na Marekani nchini Lebanon

Akiwa amevaa barakoa na vifaa kamili vya kinga binafsi, profesa anachunguza sehemu kadhaa za ganda.

Anasema, "Hii ni sehemu ya ganda la howitzer la mm 155. Kuashiria M825A1 kunaonesha kuwa ni bomu la fosforasi nyeupe. Limetengenezwa Marekani."

"Fikiria kujaribu kuondoa kemikali hii kwenye nguo zako na inaungua na kushikamana na ngozi yako."

Anasema kwamba hata baada ya siku 30, mabaki ya fosforasi nyeupe bado yanaweza kuwaka.

Je, Israel walivunja sheria?

Fosforasi nyeupe haifafanuliwi kama silaha ya kemikali, na hata neno la silaha ya moto lina utata.

Chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Silaha za Kawaida, kuna vikwazo kwa silaha iliyoundwa kimsingi kuanzisha moto au kuchoma watu.

Hatahivyo, nchi nyingi, pamoja na Israeli, zinakubali kwamba ikiwa fosforasi nyeupe inatumiwa kimsingi kuunda moshi, na sio moto (hata ikiwa utatokea kwa bahati mbaya), basi sheria ya silaha za moto haitumiki tena.

Hata hivyo, Human Rights Watch haikubaliani na maoni haya. Inasema kuna "mianya" mingi sana katika Mkataba wa Silaha za Kawaida.

"Mkataba wa Silaha za Kawaida una mianya, hasa kuhusu ufafanuzi wake wa silaha za moto," anasema Ramzi Qais, mtafiti katika Human Rights Watch.

"Lakini chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, pande zote kwenye mzozo lazima zichukue tahadhari zinazowezekana ili kuepuka kuwadhuru raia, hasa wakati wa kutumia silaha zenye fosforasi nyeupe.

"Waisraeli wanasema lengo lao lilikuwa kuunda moshi," asema Profesa Boothby. "Wanakijiji wanasema hakukuwa na madhumuni ya kuunda moshi, kwa sababu hakukuwa na watu wenye silaha. Je! hili lilikuwa kusudi la kutumia fosforasi nyeupe? Kujua jibu ni "Kwa hivyo itahitaji kujua ni nini kilikuwa kikipita akilini mwa wale waliofanya uamuzi wa kushambulia."

Profesa Boothby anasema "usawa" pia ni kipengele muhimu. Kwamba uharibifu wowote unaosababishwa sio mwingi, ukilinganisha na mafanikio ya kijeshi yanayotarajiwa.

"Tunazungumza juu ya hitaji la kuthibitisha kuwa mauaji ya raia yaliyotarajiwa, na uharibifu wa malengo ya kiraia, ulikuwa mwingi ikilinganishwa na faida halisi na ya moja kwa moja ya kijeshi ambayo walitarajia kupata kabla ya shambulio hilo.

Walipoulizwa kuhusu malengo yake, jeshi la Israel lilijibu BBC: "Haya ni mambo ya siri, na hayawezi kufichuliwa.

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Putin asaini mkataba wa kituo cha Mwezi na China