Maazimio ya Mwaka Mpya yana maana gani na kwanini tunashindwa kuyatimiza?
Kila mwaka, mamilioni ya watu hufanya maazimio ya Mwaka Mpya, wakitumaini kufanya mabadiliko chanya katika maisha yao.
Mada zinazojirudia mara nyingi huwa ni pamoja na masuala ya afya, uimarishaji wa kipato, kujifunza mambo mapya kwa maendeleo ya kibinafsi na kitaaluma na kadhalika.
Kufanya maazimio au kuweka malengo, ni kama kujiwekea muongozo wako binafsi kuhakikisha umefanikiwa.
Unapoweka malengo, unajiwekea ahadi na ndoto zako.
Yote ni kuhusu kuwajibika na kumiliki matendo yako.
Ukiwa na malengo, unajiwekea mpango wa kukuhamasisha.
Lakini kwa nini inakuwa changamoto kwa wengi kutimiza malengo waliojiwekea wenyewe?
Sababu ya kushindwa kuyafikia maazimio ya Mwaka Mpya
1. Kuweka maazimio yasiyo na uhalisia
Azimio ni kuhusu kile ambacho ungependa kufanya badala ya kile 'unachopaswa' kufanya.
Watu hujiwekea malengo magumu kupita kiasi ambayo hayafikiki haraka, au huweka malengo rahisi kiasi ambacho huchoshwa nayo wenyewe.
Ni muhimu kukagua maazimio yako ili kuona kama yanaweza kufikiwa.
Je, yanaweza kukadiriwa.
Je, pengine muda uliojiwekea kutimiza malengo unatosha?
Je, ni malengo yanayoeleweka?
Yanaendana na malengo yako?
Je, inawezekana kuyagawanya kidogo kidogo?
Je, inawezekana kuyafanikisha ndani ya muda ulioweka?
Kumbuka kwamba ili kuweka azimio, lazima ubadili tabia yako, kwa hivyo hakikisha malengo yako ni ya kuridhisha.
2. Ukosefu wa uwajibikaji
Kufanya kazi na kocha, mshauri, au mshirika wa uwajibikaji kunasaidia kuhakikisha unapata nguvu na msukumo ufaao ili kukuwezesha kuwa na ari zaidi na hata kutimiza ndoto kubwa mno.
Kwa sababu mafanikio ni jambo la muda, tunaweza kuwa na uhakika kwamba tukifuata hatua, tutafikia malengo yetu.
Epuka watu wanaokukatisha tamaa unapochagua mwenzi wako wa uwajibikaji, na badala yake fanya kazi na watu wanaokuinua na kukutia moyo, haswa unapojihisi chini.
3. Hakuna ufuatiliaji/upitiaji tena
Ukaguzi wa kila wiki au baada ya wiki mbili hukuruhusu kufuatilia maendeleo yako na kubadilisha visingizio kuwa fursa.
Kinachopimwa kinafanyika, na kile kinachofanyika kinaweza kuboreshwa na kufanywa mazoea kwa usaidizi wa mfumo mzuri wa ufuatiliaji.
Vizuizi vingi vinavyoonekana vinatokana na mawazo, makisio, hukumu, kufikiria kupita kiasi, na marejeleo ya hapo awali.
Rekodi ya mafanikio husaidia katika kuhakikisha azimio linakuwa endelevu.
4. Ukosefu wa mipango
Mipango mizuri inahitajika kila wakati kwa utekelezaji mzuri.
Ni bora zaidi ikiwa utapanga hatua za utekelezaji kuzunguka azimio lako, uyagawanye katika sehemu ndogo ndogo, na uyapange kwenye kalenda.
Malengo ya kila wiki na mipango huleta hisia ya kufanikiwa badala ya kuahirisha. Mfano, "Ohh, nina mwaka mzima, ninaweza kuanza tena mwezi ujao nikiwa na muda zaidi."
Upangaji pia huhakikisha kuwa marekebisho yote muhimu yamenakiliwa kabla ya wakati, pamoja na uelewa wa changamoto zinazowezekana kutokea.
Hii inaongeza fursa yako ya kufanikiwa, haswa linapokuja suala la malengo ya muda mrefu.
5. Kutojiamini
Usiruhusu makosa yako ya zamani kuamua maisha yako ya baadaye.
Baada ya kujifunza kutokana na kushindwa kwako, ni wakati wa kufanya kazi.
Kila ushindi mdogo unapaswa kusherehekewa kwa sababu inakupa motisha kufanya kazi kwa bidii ili upate mafanikio makubwa zaidi.
Kujikosoa au kuwa na mashaka hakusaidii kwa sababu inalenga umakini na nguvu zako zote kwenye "kwa nini siwezi kufanya hivi?"
Unapoboreka, jizoeshe kujihurumia na kujipenda, na usiruhusu kushindwa au kukatishwa tamaa kidogo kugeuka kuwa kushindwa kwa kudumu.
Kumbuka kwamba maendeleo yanafaa zaidi kuliko ukamilifu, na ikiwa unajiamini, unaweza kufikia mengi kwa kupanga vizuri, utekelezaji, kujifunza, kutafuta msaada, na mafunzo yanayofaa.
Haijalishi unahisi uzito kiasi gani, jifundishe kujitia moyo na kuendelea.
6. Ukosefu wa malengo
Watu wengi wanashindwa kufikia malengo yao kwa sababu 'malengo' yao hayajulikani.
Unaweza kujua unachotaka, lakini huwezi kujua jinsi ya kukipata hadi utakapojua kwa nini unakitaka.
Kwa hivyo, kwa nini unafanya maazimio haya? Ni swali muhimu unalofaa kujiuliza kabla ya kujiwekea malengo.
'Kwa nini' yako ina uhusiano gani wa kihisia?
Visingizio vyote hutoweka wakati madhumuni yana nguvu, na mtu hubadilika kwa kawaida kutoka kwa mtazamo usiobadilika kwenda kwa mawazo yanayotekelezeka.
Ni muhimu kuzingatia, kuchukua jukumu, kujitolea na kuelekeza umakini wote ikiwemo nguvu, mawazo na hatua ili kushikamana na maazimio ya mwaka mpya.
Yasiwe magumu sana au rahisi sana na muhimu zaidi, furahia mchakato wa mabadiliko wakati wa utekelezaji.
Kumbuka, washindi na walioshindwa wana malengo sawa; ni kile mtu anachofanya ili kujaza 'pengo' ndicho kinacholeta tofauti kubwa.