Vita vya Urusi na Ukraine: Matukio matano muhimu ya faida na hasara kwa Putin 2024
Vita vya Urusi na Ukraine: Matukio matano muhimu ya faida na hasara kwa Putin 2024

Chanzo cha picha, Reuters
Wakati 2024 inakaribia kutamatika, Rais wa Urusi Vladimir Putin alifanya mkutano kila mwisho wa mwaka huko Moscow.
Mkutano huu wa wanahabari mara nyingi hujulikana kama "maonyesho ya utendaji ya kila mwaka ya Putin." Hata hivyo, Putin anaweza kuwa amepuuza kwa makusudi baadhi ya matukio katika "onyesho la utendaji" la mwaka huu.
Hapa, tunarejea nyuma katika matukio matano muhimu yaliyoshuhudiwa katika mwaka huu kwa upande wa Putin.
Wakati wa hafla iliyoandaliwa mnamo Desemba 19, rais huyo wa Urusi alihutubia taifa juu ya maswala kadhaa, ikiwemo uchumi wa nchi hiyo, kushuka kwa viwango vya kuzaliana,Ujio wa Donald Trump na vita vya Israel-Gaza, lakini alitumia muda mwingi wa masaa manne na nusu akiangazia uvamizi unaoendelea Ukraine, vita ambavyo vinaingia katika mwaka wake wa tatu, na alitaka kuainisha juhudi za miezi 12 iliyopita kama mafanikio.
Alitangaza kwamba askari wa Urusi walikuwa "wanadhibiti na kurejesha mamlaka" na kusonga mbele"kila siku," aliwaita askari wake "mashujaa" na kujigamba kulinda uhuru wa Urusi.
Ingawa alipinga makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano, akisema alikuwa tayari kufanya "maridhiano" ili kumaliza vita, lakini haikufahamika maafikiano hayo yangehusisha nini hasa.
Alisema Kremlin ilikuwa tayari kufanya mazungumzo na Kiev bila masharti, lakini alisisitiza kutohusishwa Zelensky katika mchakato huo.
Lakini matukio matano muhimu ambayo Putin alifanya siri au kuachana nayo yalikuwa na athari gani?
Kifo cha Alexei Navalny
Mnamo Februari 16, 2024, kiongozi mashuhuri wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny, alikufa katika gereza la Siberia.
Ingawa wenzake bado wanachunguza mazingira ya kifo hicho, ni wachache nchini Urusi wanaotilia shaka kwamba kiongozi huyo wa upinzani, ambaye hapo awali aliwekewa sumu ya dawa ya neva Novichok, hakuuawa kwa amri ya Rais Vladimir Putin.
Mabadilishano makubwa ya wafungwa yalikuwa yakijadiliwa tayari huko Moscow na miji mikuu ya Ulaya, na hatimaye kufanyika mnamo Agosti 1.
Baada ya uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, ilianza pia kuwakamata raia wake waliojaribu kuleta upinzani wa aina yoyote.
Navalny mara nyingi amekuwa akipinga suala la vita, hata akiwa gerezani.
Kifo chake kilikuwa siku ya giza kwa maelfu ya watu kote Urusi.
Akikaribia kuadhimisha mwaka wa pili wa vita, baada ya makumi ya maelfu ya wanajeshi kuuawa, yaonekana rais wa Urusi aliamua kwamba mpinzani wake mkuu wa kisiasa angemwaibisha na kumuondoa.

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Mashambulizi ya Ukumbi wa Jiji la Crocus
Wakati umakini wote wa mamlaka ya Urusi unaelekezwa Ukraine, kuajiri wanajeshi zaidi na kutengeneza silaha mpya, wanaonekana kupuuza ukuaji wa hisia kali za Kiislamu katika nchi za Asia ya Kati na jamhuri za Caucasus Kaskazini za Urusi.
Mnamo Oktoba 2023, nchi hiyo ilishtushwa na shambulizi la kwenye Uwanja wa Ndege wa Makhachkala, na mnamo Machi 22, 2024, moja ya shambulio baya zaidi la kigaidi katika historia ya Urusi lilifanyika katika mkoa wa Moscow.
Shambulio la magaidi wa Kiislamu kwenye tamasha la Safranbolu City liliua watu 145 na kujeruhi 551.
Lilikuwa moja ya mashambulizi mabaya zaidi tangu kuvamiwa kwa shule ya Beslan, miaka 20 iliyopita.
Kundi la Afghanistan la Vilayat Khorasan lilidai kuhusika, lakini propaganda za Urusi, na baadaye Putin, walikimbilia kuilaumu Ukraine kwa shambulizi hilo.
Walidai kuwa washambuliaji walijaribu kukimbilia Ukraine baada ya shambulio hilo, ambalo inadaiwa lilikuwa limewaandalia njia ya kuvuka mpaka.
Kufikia mwisho wa mwaka, hakukuwa na ushahidi wowote wa kuthibitisha hili, wala haikuthibitishwa kwa njia yoyote kwamba vikosi maalum vya Ukraine vilihusika katika shambulio hilo.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba wanamgambo walijaribu kufikia Belarus ili kuendelea na safari yao kutoka huko, lakini viongozi wa Urusi mara nyingi wanailaumu Ukraine kwa matatizo yao yote.
Lakini Putin hakutaja mkasa huo katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka.

Chanzo cha picha, EPA-EFE/REX/Shutterstock
Syria: Kofi usoni
Utawala wa Bashar al-Assad ulinusurika miaka mingine tisa nchini Syria chini ya vikosi vya wanajeshi wa Urusi.
Wanajeshi wa Urusi walionekana huko mwishoni mwa 2015, na kujiimarisha kimamlaka kwa rais Assad na ushindi dhidi ya kile kinachojulikana kama Islamic State, ambayo ilipigwa marufuku nchini Urusi, kulikuzwa kwa miaka mingi na Kremlin kama moja ya mafanikio yake kidiplomasia.
Hata hivyo, kutokana na vita vya Ukraine kumeza rasilimali zake zote, Moscow haina muda tena wa kuzingatia Syria au Bashar al-Assad.
Kutokana na hali hiyo, kundi la wapiganaji wa Kiislamu la upinzani Hayat Tahrir al-Sham (HTS) liliupindua utawala wa Damascus ndani ya siku 10, na kumlazimu Assad kukimbilia Urusi kutafuta hifadhi, ambapo aliungana na kiongozi aliyetoroka Ukraine Viktor Yanukovych na wengine.
Kuanguka kwa utawala wa Assad ni habari mbaya kwa Kremlin.
Habari mbaya zaidi ni kwamba Urusi inaweza kupoteza kambi zake za kijeshi katika miji ya Syria ya Latakia na Tartus.
Hii inaweza kumaanisha kuwa Urusi italazimika kupunguza miradi yake yote ya Kiafrika na haitakuwa tena mshirika muhimu katika eneo la Mashariki ya Kati.
Kwa miaka mingi, Putin amekuwa akidai kuwa alikuwa akiirejesha Urusi katika hadhi ya ushawishi mkubwa, lakini vita na umwagaji damu vimeifanya nchi hiyo kuwa mshirika wa kanda ambayo hata majirani zake wengi hawana hamu nayo.
Hata hivyo, alisisitiza katika hotuba ya kitaifa kwamba Urusi haijashindwa nchini Syria.
Putin alisema Urusi imefanikisha malengo yake nchini Syria na kuzuia kuundwa kwa utawala wa Kiislamu, lakini amekiri kuwa hali ni mbaya.
Alisema bado hajazungumza na kiongozi wa Syria aliyetimuliwa madarakani, ambaye alikimbilia Moscow wakati waasi wakisonga mbele mjini Damascus mapema mwezi huu, lakini mazungumzo hayo yalikuwa kwenye ajenda.
Ameongeza kuwa Urusi inajadiliana na uongozi mpya wa Syria ili kubakisha vituo viwili muhimu vya kijeshi katika pwani ya Mediterania na kwamba Moscow itafikiria kuzitumia kwa malengo ya misaada ya kibinadamu.
Silaha bora,kombora la Oreshnik na chaguo lisilo la kinyuklia
Mwishoni mwa 2024, wakati wanajeshi wa Ukraine na washirika wao walipokuwa wakivuka "mstari mwekundu" wa Urusi karibu kila siku, Kremlin hatimaye ilikuja na mbinu nyingine ya chaguo la silaha ya nyuklia kutishia kila aliye karibu.
Silaha hiyo bora ni kombora la "Oreshnik".
Kombora Oreshnik limetumika mwishoni mwa Novemba katika jiji la Dnieper nchini Ukraine tu hadi sasa.
Hii inadaiwa kuandaliwa ili kukabiliana na matumizi ya kombora la masafa marefu lililotengenezwa na nchi za Magharibi kwenye eneo la Urusi.
Tangu wakati huo, Putin na propaganda za Urusi wamekuwa wakiimba sifa za kombora la Oreshnik.
Tangu silaha hiyo mpya ilipoanza kutumika, Putin ameitaja katika kila hotuba au mkutano na waandishi wa habari, na viongozi wa Jimbo la Duma wamehudhuria mikutano wakiwa wamevalia fulana zilizoandikwa neno "Oreshnik".
Hii inaweza kuonekana kama kupunguza kwa kiwango fulani cha makabiliano: angalau Kremlin inatishia maadui zake na kitu kingine isipokuwa mabomu ya nyuklia.
Kwa upande mwingine, wakati kila mtu hatimaye ataacha kuogopa kombora la Oreshnik, Kremlin inaweza kurudi kwenye matumizi ya bomu ya nyuklia tena, kwani vitisho vinaonekana kuwa mbinu ya kawaida ya Rais Putin.
Urafiki na Kim Jong-un

Chanzo cha picha, SPUTNIK/KREMLIN POOL/EPA-EFE/REX/Shutterstock
Mwishoni mwa 2023, Kremlin ilianzisha ushirikiano wa kijeshi na Korea Kaskazini. Hapo awali, Urusi, pamoja na wanachama wengine wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, walikuwa wameiwekea vikwazo Korea Kaskazini.
Hapo awali, kwa sababu ya uhaba wa sialaha na makombora ya masafa marefu katika vita na Ukraine, Moscow ilianza kupata silaha hizo kutoka Pyongyang. Kwa kubadilishana, Urusi iliipatia Korea Kaskazini mafuta ili kukwepa vikwazo.
Mnamo 2024, Putin alikutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un huko Pyongyang.
Mara ya mwisho kutembelea mojawapo ya tawala za kidikteta zinazokandamiza zaidi duniani ilikuwa mwaka 2000, wakati Korea Kaskazini ilipoongozwa na babake Kim Jong-un, Kim Jong-il.
Lakini huko Urusi, kwa miaka mingi, mtu mmoja tu ndiye amekuwa madarakani.
Baada ya wawili hao kukutana, nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya "ushirikiano wa kimkakati wa kina".
Miongoni mwa mambo mengi, zilikubaliana kusaidiana kijeshi "ikiwa upande wowote ulijikuta katika hali ya vita." askari wa Korea Kaskazini walionekana kwenye mstari wa mbele.
NATO inataja idadi yao kuwa karibu 12,000, tathmini sawa na iliyotolewa na mamlaka ya Ukraine.
Awali Moscow na Pyongyang zilikanusha kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini walihusika katika vita vya Ukraine, huku kauli ya kawaida ikiwa "hawapo."
Mwishoni mwa Oktoba, akizungumzia ukweli kwamba Urusi sasa inapokea sio tu risasi bali pia wafanyakazi kutoka Korea Kaskazini, Putin alitaja makubaliano ya "ushirikiano wa kimkakati" ambayo yamefikiwa, akisema "tutakachofanya na jinsi tutakavyofanya ni juu yetu''.
Ujumbe wa wanajeshi wa Korea Kaskazini ulijaribu kutwaa tena ardhi katika eneo la Kursk ambalo Ukraine ilikuwa ilichukua mwezi Agosti.
Kufikia Desemba, mamia ya Wakorea Kaskazini walikuwa wameripotiwa kufariki na kujeruhiwa.
Hii ilikuwa vita ambayo watu wao labda hawakuijua hadi hivi karibuni - magazeti ya nchini humo hayakuripoti juu yake katika mwaka wa kwanza.
NATO inachukulia kujihusisha kwa Korea Kaskazini katika vita vya Ukraine kama ongezeko la wazi kwa sababu Urusi inaingiza moja kwa moja mshirika wa tatu katika mzozo huo.
Chanzo kimoja cha BBC kutoka NATO pia kilidokeza kwamba matokeo ya hatua hii yataathiri zaidi hali ya uwanja wa vita.
Marekani inaamini kwamba mshirika mwingine muhimu wa Urusi, China, hajafurahishwa na kukua kwa urafiki kati ya Moscow na Pyongyang.