Simulizi za wanawake waliozuiliwa katika jela mbaya ya Evin ya Iran
- Author, BBC 100 Women
- Nafasi,
Akiwa ameketi peke yake chini, ndani ya seli ndogo isiyo na madirisha, Nasim alisikia sauti za mateso kutoka kwa wafungwa wengine.
Mlinzi angegonga mlango wake na kusema: "Unasikia hicho kichapo? Jiandae, wewe ndiye unafuata."
Alikuwa "akichunguzwa kwa saa 10 hadi 12 kila siku" na alitishiwa mara kwa mara na adhabu ya kuuawa.
Mahabusu hiyo ilikosa vifaa vya msingi, kama vile kitanda au choo, na ilikuwa na ukubwa wa mita mbili tu.
Miezi minne ya kifungo cha peke yake ilikuwa ni utangulizi wa Nasim, msusi mwenye umri wa miaka 36, katika jela maarufu ya Evin.
Aliishi akiwaona tu waliokuwa wakimuadhibu. Aliamini kwamba "atafariki na hakuna atakayejua."
Tumekusanya simulizi kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika ili kuunda picha ya maisha ya kila siku kwa Nasim na wanawake wengine, ambao sasa wanashikiliwa katika jela ya Evin.
Wengi wao walikuwa miongoni mwa maelfu ya watu waliokamatwa kuhusiana na maandamano ya "Wanawake, Maisha, Uhuru" yaliyochochewa na kifo cha Mahsa Amini, msichana wa miaka 22 aliyeuwawa mnamo Septemba 2022.
Mahsa alikamatwa kwa tuhuma za kuvunja sheria za Iran zinazotaka wanawake kuvaa hijabu, na alikufa akiwa mikononi mwa polisi.
Ingawa watu wamezungumza kuhusu hali za Evin baada ya kuachiliwa, ni nadra kupata maelezo kuhusu maisha ya wafungwa wakiwa bado ndani.
Tunachokiskia kinatuchorea taswira kamili ya ukatili unaoendelea katika jela hiyo ,kampeini za kutaka haki za wanawake ziheshimiwe pamoja n avikwazo wanavyowekewa wakisubiri vifungo vyao.
Cha kustaajabisha zaidi ni kuwa baadhi ya wanawake hao wanaruhusiwa kujamiiana na waume zao hadi kushika mimba.
Nasim-ambaye anapenda nyimbo za kufoka na kujipodoa-aliletwa katika jela hiyo mwezi Aprili 2023 baada ya kuandamana akiwa na marafiki zake ,mmoja wao akiuawa katika maandamano hayo.
Baada ya kuachiliwa huru kutoka kwa jela hiyo waliomuona walisema alikuwa na majeraha mengi mwilini akisema aliyapata wakati alipolazimishwa kukiri makosa yakusingiziwa.
Naye Rezvaneh alikamatwa pamoja na mumewe wakati wa maandamano mwaka wa 2023.
Walinzi wa jela hiyo walikuwa wakimtishia maisha jinsi watakabvyomuadhibu mumewe na kumuumiza vibaya.
Ni seli kama hiyo ambapo raia waUingereza na Iran Nazanin Zaghari- Ratcilffe ,alikuwa amezuiliwa kwa miaka minne kabla ya kuachiliwa huru na kurejea Uingereza mwaka 2022.
Wanawake wengi waliozuiliwa kwa jela hii ni kutokana na uanaharakati wao ,kusambaza propaganda , kukosoa utawala wa nchi hiyo na pia madai ya kuhatarisha usalama wa taifa.
Wanaishi kwa seli nne ambazo zimejaa pomoni kila mahabusu ikiwa na wanawake 20 na vitanda pekee.
Wakiishi kwa pamoja kuna wakati hukosana na pia kushirikiana na kuwa marafiki.
Katika jela ya Evin, hali ya maisha kwa wanawake ni ya kipekee na yenye changamoto kubwa.
Msimu wa baridi kila mmoja hujikinga baridi kuingia mwilini kwa kubeba chupa zilizojaa maji moto na wakati wa joto ni kuhangaika na jasho mwilini .
Pia Kuna sehemu ndogo ya jikoni, na majiko machache ambapo - ikiwa wana fedha za kutosha kununua chakula kutoka kwa duka liliko kwa jela - wanawake wanaweza kupika vyakula vyao wenyewe ili kuongeza kiwango cha chakula cha kila siku kinachotolewa na gereza.
Hata hivyo, mazingira haya ni magumu, na chakula wanachopatiwa ni cha msingi tu, kilichokosa ladha na hakina virutubisho vya kutosha.
Wanawake wanaruhusiwa kuvaa mavazi yao ya kawaida na kuzunguka ndani ya vyumba vyao vya kulala ambavyo vina vyumba viwili vya kuoga.
Kila jioni, wanapanga foleni ili kutumia choo na kusafisha meno yao.
Rezvaneh ambaye alikuwa na matatizo ya kutopata ujauzito siku moja akijifanyia usafi aligundua yeye ni mjamzito.
Akiwa na mumewe ambaye pia ni mfungwa katika jela hiyo alikuwa akiruhusiwa kukutana faragha na sasa ana mimba.
Japokuwa ni habari njema kwa ndoa yake aliingiwa na hofu akieleza kuwa jela hiyo haikuwa na mazingira mazuri ya kulea mimba.
Anaeleza kuwa kuna wakati alikuwa na umito wa kunywa sharubati ya tufaha,nyama na pia mkate lakini haingewezekana kutokana na bei kuwa ghali mno.
Alipofikisha miezi minne aliruhusiwa kufanyiwa uchunguzi na daktari wa uzazi na kugundua alikuwa amebeba mtoto wa kike.
Hali yake ya afya haikuwa sawa kwani ana kifafa na madaktari katika jela walimsihi asijizonge na mawazo kwani huenda mimba ikachomoka.
Vida, ambaye ni mwanahabari ,na anapenda uchoraji, wakati wake mwingi hutumia kuchora wanawake wengine akitumia shuka kama turubai ya kuchorea picha.
Picha moja ambayo ilitolewa nje ya jela , alikuwa amemchora mfungwa wa asili ya kurdi Pakhshan Azizi ambaye alikuwa akizunguka Iraq na Syria kuwasaidia waathiriwa wa kundi la kigaidi la IS.
Pakhshan amehukumiwa kifungo cha kuuawa na huenda kikatekelezwa wakati wowote kutoka sasa.
Hata hivyo Vida ameagizwa asichore picha ambayo ina maana fiche.
Kwa mfano kuna picha alichora ukutani mawe yaliyoanguka nyuma yake kukiwa na msitu uliojaa miti .Mamlaka iliziba picha hiyo.
Pia kuna picha alichora ya chui ukutani katika ushoroba wa jela hiyo ambapo wanawake walimsifia kuwa picha hiyo iliwapa ukakamavu na kutokana na hili maamlaka ilifuta.
Lakini kuna baadhi ya kazi zake bado zipo -kuna mchoro wa mawimbi ya bahari ya buluu ambapo ni sehemu iliyotengewa wanawake wakavute sigara.
Kupata huduma za matibabu imekuwa changamoto kubwa kwa wanawake hawa waliozuiliwa kwa jela hii maarufu nchini Iran.
Mmoja wa wafungwa, mwanaharakati wa haki za binadamu na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Narges Mohammadi, ana matatizo ya moyo na mapafu ambayo ni hatarishi kwa maisha yake.
Lakini gerezani, alikataliwa kupata matibabu kutokana na msimamo wake wakukataa kuvaa hijabu anapokwenda kupata matibabu hospitalini.
Walikubali tu baada ya wafungwa wenzake kuanza mgomo wa kususia chakula kwa wiki mbili.
Hatimaye, Narges alikubaliwa kutoka gerezani kwa siku 21 mwanzoni mwa mwezi Disemba kwa misingi ya kiafya.
Katika gereza, yeye na wanawake wengine wamekuwa wakifanya maandamano, ya kupigani haki zao kama wanawake.
Ingawa sheria inawahitaji kuvaa hijabu, wengi wao wanakataa.
Baada ya mapambano marefu na mamlaka, wanawake waliruhusiwa kuweka mapazia kando ya vitanda vyao ili waweze kuwa na faragha, mbali na macho ya kamera za CCTV.
Moja ya mambo magumu zaidi kwa wanawake hawa ni kungojea hukumu zao.
Walinzi waliokuwa wamemzuia Nasim walimtishia adhabu ya kifo, na alilazimika kusubiri takribani siku 500 ili kujua hatma yake.
Katika hali ngumu, alikuta faraja kwa wenzake wa gerezani - ambao aliwaita kama "dada" ambao walimpa nguvu ya kuishi na kumtibu majeraha ya kiakili na kihisia. Kila asubuhi, mmoja wa marafiki zake alikua akivua pazia la kitanda na kumlazimisha amke kwa ajili ya kifungua kinywa.
"Kwa kila siku, tunatafuta jambo fulani la kufanya ili mwishowe waweza kusema, 'Leo tumeishi,'" alielezea mmoja wa vyanzo vyetu.
Wanawake wengine hutumia muda wao kusoma mashairi, kuimba, kucheza michezo ya karata wakiwa wamezitengeneza wenyewe, na kutazama televisheni - kuna televisheni mbili ambapo wanaweza kutazama vipindi vya irani, vipindi vya tamthilia, makala maalum na soka.
Hii ndiyo ilikuwa mtindo unaowasaidia wanawake kama Nasim kuendelea na maisha huku wakisubiri hukumu zao, huku wakikabiliwa na tishio la daima la adhabu ya kifo.
Na wakati hukumu ilipotolewa, Nasim alikabidhiwa adhabu ya miaka sita gerezani, vipigo 74 vya mijeledi, na miaka 20 ya uhamisho katika kijiji kidogo mbali na Tehran. Alihukumiwa kwa usambazaji wa propaganda na kuchora silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Licha ya ukali wa adhabu, Nasim alijisikia kama yupo huru tena, na kuweza kufurahia maisha tena aliyoona kuwa ameyapoteza.
Wanawake wengine wanne katika kifungo hicho walihukumiwa kifo kwa sababu ya kuchora silaha dhidi ya utawala au kushirikiana na makundi ya wanamgambo.
Hata hivyo, mmoja wao alifutiwa hukumu yake.
Zaidi ya watu 800 waliuawa kwa kifo mwaka jana nchini Iran, ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika miaka nane, kulingana na Amnesty International.
Wengi walikuwa na mashtaka ya unyanyasaji wa nguvu na dawa za kulevya, huku wachache wakiwa ni wanawake.
Hivyo, kila Jumanne, wanawake hao hufanya maandamano dhidi ya hukumu za kifo, wakipiga nduru katika uwanja wa gereza, wakikataa kuondoka usiku mzima na kuanzisha mgomo wa kususia chakula.
Kampeni hii imeenea katika magereza kote Iran, na kupata msaada wa kimataifa.
Katika maadhimisho ya kifo cha Mahsa Amini, wanawake walichoma hijabu zao kuonyesha wameghadhabika.
Lakini, maisha ya kikatili hayajawakatiza tamaa ya kupigania haki za wanawake hawa.
Walikumbana na ukatili - mara nyingi walishambuliwa na walinzi, kupigwa na kujeruhiwa.
Walinzi wengi ni wanawake, na "wengine wao ni wema, wengine ni wakali na wasio na huruma, kulingana na maagizo wanayopokea kutoka kwa mamlaka ya juu," asema mmoja wa vyanzo vyetu.
Serikali ya Iran mara nyingi inakana tuhuma za ukiukaji wa haki za binadamu, ikisema kwamba hali ndani ya gereza la Evin inakidhi viwango vyote muhimu na wafungwa hawatendewi ukatili.
Wakati tarehe ya kujifungua ilikaribia kwa Rezvaneh, mamlaka za gereza zilimruhusu kuondoka gerezani kwa muda ili kujifungua.
Mwezi Oktoba, alijifungua mtoto wa kike.
Lakini furaha na faraja yake ya kumkaribisha mtoto wake salama ilikuwa imejaa hofu, huzuni, na hasira.
Mumewe hakuruhusiwa kutoka gerezani na yeye, ingawa aliruhusiwa kumtembelea mtoto wao gerezani.
Na kwa sababu ya msongo wa mawazo, Rezvaneh hajaweza kupata maziwa ya kutosha ya kumyonyeshea mtoto wake aliyemsubiri kwa hamu.
Anatarajiwa kurudi gerezani hivi karibuni akiwa na mtoto wake mchanga ili kumalizia kifungo chake cha miaka mitano - ikiwa hatapewa msamaha mapema, hiyo inaweza kuwa takribani miaka minne.
Watoto kawaida huruhusiwa kubaki na akina mama wao gerezani hadi wanapofikia umri wa miaka miwili.
Baada ya hapo, mara nyingi hupelekwa kwa jamaa wa karibu, au ikiwa hilo haliwezekani, hupelekwa katika hifadhi ya watoto.
Lakini badala ya kuwakatisha tamaa, mmoja wa wafungwa amesema changamoto wanazozikabili zimewafanya "kuwa jasiri na wenye nguvu zaidi," wakisaidia imani yao kwamba "mustakabali uko wazi: kupigana, hata gerezani."