Mtanziko wa ANC katika kuamua mustakabali wa Afrika Kusini

 O

Chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress (ANC), kinakabiliwa na kizungumkuti juu ya mustakabali wa nchi hiyo baada ya kupoteza idadi kubwa ya wabunge katika uchaguzi wa wiki iliyopita.

Kimeshinda kwa asilimia 40 ya kura, ANC inahitaji kupata mshirika ili kupata wingi wa wabunge ambao wataunga mkono rais atakae chaguliwa – ama iamue kwenda peke yake na serikali ya wachache.

Chaguo moja litakuwa, ni kufanya makubaliano na chama cha pili kwa ukubwa, chama cha mrengo wa kati cha Democratic Alliance (DA), ambacho kilipata 22% ya kura.

Wapo wenye matarajio ya kuona muungano wa ANC-DA, hasa kwa vile unapendelewa na sekta binafsi kama chaguo bora zaidi la kuhakikisha uthabiti wa kiuchumi.

Hata hivyo hilo linaweza kuwa hatari kisiasa, kwani wakosoaji wa DA wanakishutumu kwa kujaribu kulinda uchumi wa wazungu wachache – walioupata wakati wa mfumo wa ubaguzi wa rangi - madai ambayo chama hicho kinakanusha.

Vinginevyo, ANC inaweza kufanya kazi na vyama viwili vyenye itikadi kali - chama cha Rais wa zamani Jacob Zuma cha Umkhonto weSizwe (MK) au Economic Freedom Fighters (EFF) cha Julius Malema.

Vyama hivi vitatu vina ngome zao katika majimbo yenye watu wengi weusi, na kura zao kwa pamoja zinafikia 65%. Malema ameionya ANC dhidi ya kuunda muungano ambao "utaimarisha ukuu wa wazungu" na kuwa "kibaraka wa ajenda ya ubeberu wa kizungu."

ANC na DA?

Sera za DA zinapingana kwa kiasi kikubwa na za ANC, lakini vyote vinakubaliana juu ya haja ya kufuata katiba ya sasa, ambayo Afrika Kusini iliipitisha mwishoni mwa ubaguzi wa rangi mwaka 1994.

Rais Cyril Ramaphosa ameweka wazi, makubaliano yoyote yatalazimika kuwa ndani ya mfumo wa katiba ya sasa.

Moja ya vikwazo vikubwa kwa ANC na DA, ni upinzani mkali wa DA wa sera za ANC katika huduma ya afya, ambayo itafadhiliwa na serikali, DA inakataa, ikisema ni ghali sana na inatishia mustakabali wa taasisi binafsi za afya.

DA inaamini katika soko huria, inapinga kima cha chini cha mshahara, na inataka kupunguza urasimu, ikisema hizo ndiyo njia bora za kuboresha uchumi na kuinua viwango vya maisha kwa Waafrika Kusini wote.

Inapinga vikali sera za ANC za kuwawezesha watu weusi kiuchumi, inaziona kuwa zinabagua watu wa rangi nyingine, huku zikiongeza tu kuwatajirisha wafanyabiashara wa ANC.

ANC imekanusha madai hayo, na imetekeleza sera hiyo kikamilifu, ikisema inawapa watu weusi sehemu ya uchumi ambayo walinyimwa wakati wa ubaguzi wa rangi.

Mwenyekiti wa ANC Gwede Mantashe amekwenda mbali na kusema sera za ANC za kuwawezesha watu weusi haziwezi kujadiliwa.

Kulingana na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani, Rais Ramaphosa yuko tayari kuingia katika muungano na DA, akiamini tofauti zao za kisera zinaweza kuondoshwa.

ANC na MK?

RF

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Rais wa zamani Jacob Zuma alisababisha mshtuko baada ya chama chake kushika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo

Chaguo jingine la ANC ni kuunda muungano na MK, kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi kwa kupata nafasi ya tatu kwa 15% ya kura katika uchaguzi wa kwanza ilioshiriki.

Lakini kinataka kura zipigwe tena, kwa madai kwamba kilipata kura nyingi zaidi lakini matokeo ya mwisho yalichakachuliwa. Tume ya uchaguzi imekataa madai hayo, na MK bado haijawasilisha ushahidi wowote kuunga mkono madai yake.

Pengo kati yake na ANC ni pana, pana kuliko chama kingine chochote, kwa sababu ya uhasama binafsi kati ya Zuma na Ramaphosa, ambaye alimtoa madarakani kama kiongozi wa nchi.

Pamoja na kutaka rais mpya, MK pia inataka katiba kuvunjwa ili Afrika Kusini iwe na "bunge huru la kidemokrasia" - jambo ambalo ANC imelikataa.

ANC na EFF?

Kwa mtazamo wa awali, EFF pia nayo inaondoka katika muungano, kwani inadai marekebisho ya katiba ili ardhi inayomilikiwa na wazungu iweza kugaiwa bila kulipiwa fidia.

Malema, kiongozi wa zamani wa vijana wa ANC ambaye alifukuzwa na chama mwaka 2012 kwa kuzua migawanyiko na kukipa chama sifa mbaya, alisema, “EFF iko tayari kufanya kazi na ANC katika serikali ya mseto.”

Hata hivyo, madai ya chama hicho ya mgawanyo wa ardhi, ndio "sera muhimu," na haitajiunga na serikali ikiwa ANC itaikataa.

ANC na EFF kwa pamoja wana viti 198 - pungufu ya viti 201 vinavyohitajika kuwa na wingi bungeni, hivyo chama kingine kidogo kitalazimika kuletwa katika muungano huo.

Viongozi wa ANC huko Gauteng - jimbo kubwa na tajiri la Afrika Kusini - inaelezwa wanapendelea makubaliano na EFF, lakini upendeleo huo umedhoofika sana kutokana na ukweli kwamba vyama hivyo viwili havina viti vya kutosha kuwa na wingi wa wabunge.

Au wanaweza kuungana na MK ya Zuma, ambayo pia inaunga mkono ugawajwi wa ardhi, na kinasema kuna haja ya kugawanywa mashamba kwa "usawa miongoni mwa wakulima."

ANC, EFF na MK?

DF

Chanzo cha picha, REUTERS

Maelezo ya picha, Chama cha Economic Freedom Fighters cha Julius Malema kilipoteza kura katika uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Mei

Lakini ili kubadili katiba, theluthi mbili inahitajika na huku ANC, EFF na MK wanapungukiwa na viti 267 vinavyohitajika - wana viti 256 kwa pamoja.

Ingawa ANC inapinga marekebisho ya katiba, inakubali kwamba mifumo ya sasa ya umiliki wa ardhi unahitaji kushughulikiwa.

Katika mahojiano na gazeti la Sunday Times la Afrika Kusini, Rais wa zamani Kgalema Motlanthe, mshirika wa karibu wa Ramaphosa, alisema "swali la ardhi" lilikuwa "chanzo cha malalamiko ya kitaifa."

Maoni yake yanaonyesha kuwa kunaweza kuwa na nafasi ya makubaliano na EFF, na pengine hata MK, kuhusu suala hilo.

DA inapinga vikali makubaliano kati ya wapinzani wake watatu, ikisema utakuwa "Muungano wa Siku ya Mwisho" ambao utaigeuza Afrika Kusini kuwa "Zimbabwe au Venezuela."

"Muungano huo utaitumbukiza nchi hii katika migogoro ya kikabila na rangi ambayo haijawahi kushuhudiwa hapo awali," chama hicho kinasema.

Lakini baadhi ya maofisa wa ANC wana maoni tofauti - wanaamini kutakosekana utulivu ikiwa MK itatengwa, kutokana na mafanikio yake katika uchaguzi, ambayo yamekifanya kuwa chama kikubwa zaidi huko KwaZulu-Natal.

KwaZulu-Natal ni jimbo la pili la Afrika Kusini kwa idadi kubwa ya watu, na mara nyingi huelezwa kuwa ndio mshipa wa uchumi wa taifa hilo kwa sababu ya bandari zake.

Pia ni jimbo lenye hali tete kisiasa, likiwa na historia ya ghasia - zaidi ya watu 300 walikufa katika ghasia baada ya Zuma kufungwa gerezani mwaka 2021.

Alipatikana na hatia ya kudharau mahakama kwa kukaidi agizo la kutoa ushirikiano katika uchunguzi rasmi wa ufisadi katika kipindi chake cha urais wa miaka tisa, uliokamilika 2018.

Zuma anatazamiwa kufikishwa mahakamani mwaka ujao kwa tuhuma za ufisadi kuhusu mkataba wa silaha wa 1999 – na kuna hatari ya wimbi jipya la ghasia.

Maofisa hao wanaona aina fulani ya makubaliano yanahitajika kuafikiwa, ili kumaliza jambo hilo na kuitambua hadhi yake kama rais wa zamani.

Serikali ya Wachache?

Tovuti ya News24 ya Afrika Kusini inaripoti kuwa ANC inazingatia chaguo la kuunda serikali ya wachache, huku ikitia saini makubaliano ya kuungwa mkono na DA katika mambo muhimu, na chama cha weusi cha Inkatha Freedom Party, kinachoungwa mkono KwaZulu-Natal, jimbo lenye viti 17.

Vyama hivyo viwili vitapiga kura na ANC katika masuala muhimu kama vile bajeti, wakati ANC ikilazimika kuvishawishi vyama hivyo kila mara na vyama vingine kuunga mkono sheria nyingine.

Hilo linaweza kuisaidia ANC kutoka katika mtanziko wake wa kuchagua mshirika wa muungano, na hilo pia linaweza kuwa jambo bora kwa DA, kwani kuungana na ANC kunaweza kusababisha kukosa uungwaji mkono.

Hata hivyo, kuna hatari kwamba serikali ya wachache inaweza kusababisha kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na "siasa za miamala” - wabunge wa upinzani watakapo dai au kupewa hongo ili kuunga mkono sheria inayofadhiliwa na ANC.

Bado ni mapema sana kusema nini kitatokea, lakini Waafrika Kusini wengi wanatumai wakati bunge litakapokutana, ndani ya wiki mbili, kutakuwa na mpango wa jinsi serikali ijayo itakavyokuwa.

 

Popular posts from this blog

Jeshi la Wanamaji la Marekani limesema linakabiliwa na vita 'kali zaidi' tangu Vita vya Pili vya Dunia dhidi ya Wayemeni

Hamas yadai kuwakamata wanajeshi wa Israel lakini Israel imekanusha madai hayo