Biden 'hana imani' ya kufanyika kwa makabidhiano ya amani ikiwa Trump atashindwa
Biden 'hana imani' ya kufanyika kwa makabidhiano ya amani ikiwa Trump atashindwa

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Marekani Joe Biden amesema hana imani kuwa kutakuwa na mpito wa amani iwapo Donald Trump atashindwa katika uchaguzi wa urais mwezi Novemba.
Katika mahojiano yake ya kwanza tangu alipojiondoa katika kinyang'anyiro hicho mwezi uliopita, Bw Biden aliambia CBS News: "Ikiwa Trump atashindwa, sina imani hata kidogo." "[Trump] anamaanisha anachosema, hatumchukulii kwa uzito.
Anamaanisha hivyo, mambo haya yote kuhusu 'tukishindwa kutakuwa na umwagaji damu'."
Maoni ya Bw Trump kwamba "kutakuwa na umwagaji damu nchini" ikiwa atashindwa katika uchaguzi, yaliyotolewa alipokuwa akizungumzia sekta ya magari mwezi Machi, yalizua wimbi la ukosoaji.
Wanademokrats walikariri ujumbe wao wa kampeni kwamba rais huyo wa zamani ni tishio kwa demokrasia.
Kampeni ya Biden ilitumia maoni ya "umwagaji damu" katika tangazo - lililotumwa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii na msemaji alimshutumu Bw Trump kwa "kuhimiza na vurugu za kisiasa".
Kampeni ya Trump, hata hivyo, ilisema maoni hayo yalihusu tasnia ya magari na yametolewa kimakusudi nje ya muktadha.