Hamas yamtangaza Yahya Sinwar kuwa kiongozi mpya wa kundi hilo
Hamas yamtangaza Yahya Sinwar kuwa kiongozi mpya wa kundi hilo

Chanzo cha picha, EPA
Baada ya siku mbili za mazungumzo marefu huko Doha, Hamas imemteua Yahya Sinwar kuwa mkuu wake mpya, akichukua nafasi ya Ismail Haniyeh aliyeuawa mjini Tehran juma lililopita.
Tangu 2017, Sinwar amehudumu kama kiongozi wa kikundi ndani ya ukanda wa Gaza. Sasa atakuwa kiongozi wa mrengo wake wa kisiasa.
Uongozi wa Hamas kwa kauli moja umemchagua Sinwar kuongoza vuguvugu hilo, afisa mkuu wa Hamas aliiambia BBC.
Tangazo hilo linakuja wakati ambapo hali ya wasiwasi inaongezeka katika eneo la Mashariki ya Kati, huku Iran na washirika wake wakitishia kulipiza kisasi mauaji ya Haniyeh, ambayo wanailaumu Israel. Israel haijatoa kauli yoyote kuhusu hilo.
Kwa muda wa siku mbili huko Doha, mikutano iliyohusisha viongozi wakuu wa Hamas ilitoa uamuzi kuhusu kiongozi anayefuata wa kikundi.
Matukio mengi yalijadiliwa, lakini hatimaye, majina mawili tu yaliwekwa mbele: Yahya Sinwar, na Mohammed Hassan Darwish.
Baraza hilo lilipiga kura kwa kauli moja kumchagua Sinwar, katika kile afisa mmoja wa Hamas alielezea kwa BBC kama "ujumbe wa dharau kwa Israel". "Walimuua Haniyeh, mtu aliyebadilika ambaye alikuwa tayari kupata suluhu. Sasa wanapaswa kukabiliana na Sinwar na uongozi wa kijeshi,” afisa huyo alisema.
Kabla ya kifo chake, Ismail Haniyeh alitazamwa na wanadiplomasia wa kikanda kama mtu wa vitendo ikilinganishwa na wengine katika Hamas, kichocheo kikuu cha mawasiliano ya kisiasa ya kundi hilo.