HAMAS: Hatutashiriki mazungumzo ya usitishaji vita Doha
HAMAS: Hatutashiriki mazungumzo ya usitishaji vita Doha
Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) amesema wawakilishi wa harakati hiyo ya muqawama hawatashiriki mazungumzo ya leo ya usitishaji vita yanayotazamiwa kufanyika Doha, mji mkuu wa Qatar.
Televisheni ya Al-Mayadeen ya Lebanon jana Jumatano ilimnukuu afisa huyo wa ngazi ya juu wa HAMAS ambaye hakutaka kutaja jina lake akisema kuwa, wawakilishi wa harakati hiyo hawatahudhuria kikao cha leo Alkhamisi cha Doha, cha kujadili usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza na makubaliano ya kubadilishana mateka, kutokana na hujuma za kikatili za utawala wa Kizayuni na Waziri Mkuu wake Benjamin Netanyahu huko Gaza.
Afisa huyo wa HAMAS anasisitiza kwamba, kundi hilo la muqawama halitakubali kuanza kwa mazungumzo mapya huko Doha bila ya upande mwingine kuzingatia mapendekezo yaliyowasilishwa Julai 2.
HAMAS Jumapili usiku wiki hii ilitoa taarifa ikisisitiza kuwa, vipengee vilivyofikiwa katika mapatano ya awali vinapasa kutekelezwa kwanza badala ya kuanza mazungumzo mapya ya kusimamisha vita huko Gaza na kuzitaka pande suluhushi kuja na mpango kwa mujibu wa mazungumzo ya awali.
Afisa huyo mwandamizi wa HAMAS pia ameiambia Al-Mayadeen kuwa, Netanyahu ameweka masharti mapya ambayo yatavuruga mchakato wa mazungumzo hayo.
Hii ni katika hali ambayo, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya
HAMAS awali alisema kuwa kushiriki kwao katika mazungumzo ya Doha
kunategemea na kusimamishwa vita katika Ukanda wa Gaza. Yahya Sinwar
ametuma ujumbe kwa ajili ya usuluhishi na akasema utawala wa Kizyauni
unapasa kusitisha harakati zake za kijeshi katika Ukanda wa Gaza kama
kweli unataka kufikiwa mapatano.