Kamala Harris asema vifo vya raia ni 'vingi sana' Gaza
Kamala Harris asema vifo vya raia ni 'vingi sana' Gaza

Chanzo cha picha, MAHMOUD ZAKI/EPA-EFE/REX/Shutterstock
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amelaani kupoteza maisha ya raia katika shambulio la anga la Israel dhidi ya jengo la shule huko Gaza siku ya Jumamosi.
Zaidi ya watu 70 waliuawa katika jengo lililokuwa likiwahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao, mkurugenzi wa hospitali moja ameiambia BBC.
Bi Harris alisema raia "wengi sana" wameuawa "bado tena" na akasisitiza wito wa makubaliano ya kutekwa nyara na kusitishwa kwa mapigano, akirejea maoni yaliyotolewa na Ikulu ya Marekani.
Msemaji wa jeshi la Israel amesema shule ya al-Taba’een "inatumika kama kituo cha kijeshi cha Hamas na Islamic Jihad", jambo ambalo Hamas inakanusha.
Akizungumza katika kampeni huko Phoenix, Arizona, Bi Harris alisema Israel ilikuwa na haki ya "kuwafuata Hamas" lakini pia ina "jukumu muhimu" ili kuepuka madhara kwa raia.
Shambulio la anga la Jumamosi limekosolewa na mataifa yenye nguvu ya Magharibi na kikanda, huku Misri ikisema ilionesha kuwa Israel haina nia ya kufikia usitishaji vita au kumaliza vita vya Gaza.
Fadl Naeem, mkuu wa Hospitali ya al-Ahli ambako wengi wa majeruhi walipelekwa, alisema karibu waathiriwa 70 walitambuliwa saa chache baada ya shambulio hilo, huku mabaki ya wengine wengi yakiwa yameharibika vibaya kiasi kwamba utambuzi ulikuwa mgumu.
Jeshi la Israel lilisema "limewashambulia haswa magaidi wa Hamas wanaoendesha shughuli zao ndani ya kituo cha udhibiti wa Hamas kilichowekwa katika shule ya al-Taba'een".
Taarifa ya Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) na Shirika la Usalama la Israel ilisema "takribani magaidi 19 wa Hamas na Islamic Jihad" "walitokomezwa" katika shambulio hilo.
Msemaji wa IDF Adm Daniel Hagari alisema "dalili mbalimbali za kijasusi" zinaonesha "uwezekano mkubwa" kwamba kamanda wa Kikosi cha Kambi Kuu cha Islamic Jihad, Ashraf Juda, alikuwa katika shule ya Taba'een ilipopigwa. Alisema bado haijabainika iwapo kamanda huyo aliuawa katika shambulio hilo.