Maandamano makubwa yafanyika kila pembe ya dunia kulaani mauaji ya kinyama katika Skuli ya Al-Tabeen, Ghaza
Maandamano makubwa yafanyika kila pembe ya dunia kulaani mauaji ya kinyama katika Skuli ya Al-Tabeen, Ghaza
Watu katika nchi na mataifa mbalimbali duniani wameandamana kulalamikia na kulaani mauaji ya kimbari na ya kinyama ya Wapalestina yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Skuli ya Al-Tabeen katika Ukanda wa Ghaza.
Siku ya Jumapili mtandao wa Telegram wa Kanali ya Quds News
ulionyesha picha za maandamano makubwa ya wananchi wa Canada ya kulaani
jinai za utawala wa Kizayuni katika Skuli ya Al-Tabaeen katika mji wa
Ghaza, ambapo waandamanaji hao walipiga nara za kulaani jinai za utawala
wa Kizayuni za kuwaua wanawake na watoto wasio na ulinzi.
Ukurasa wa mtumiaji mmoja wa Palestine Online nao pia ulionyesha
katika mtandao wa kijamii wa X taswira za maandamano ya watetezi na
waungaji mkono wa Palestina katika mji mkuu wa Malaysia, Kuala Lumpur,
ambapo washiriki wa maandamano hayo wameonyesha mshikamano wao na watu
wa Palestina na kutaka kukomeshwa mauaji ya kimbari yanayoendelea
kufanywa katika Ukanda wa Ghaza.
Waungaji mkono kadhaa wa Palestina katika miji ya Gothenburg na
Stockholm nchini Sweden, katika miji kadhaa ya Uholanzi na jiji la
Manchester, nchini Uingereza, nao pia waliandamana kuonyesha mshikamano
na watu wa Palestina.
Huko Amman, mji mkuu wa Jordan, watu walikusanyika karibu na
ubalozi wa utawala wa Kizayuni na kulaani mashambulizi ya utawala wa
Kizayuni katika Skuli ya Al-Tabeen huko Ukanda wa Ghaza.

Waandamanaji walitoa nara za "Waliokuwa wakisali wamekufa shahidi, ni aibu kwa wale wanaochukua hatua ya kuanzisha uhusiano (na Wazayuni)".
Nchini Morocco pia wananchi waliandamana kupinga mauaji ya kinyama
ya Wazayuni katika kambi za wakimbizi wa Kipalestina huko Ghaza.
Huku wakiwa wamebeba bendera za Palestina, waandamanaji hao walitoa
nara za "Roho zetu na nafsi zetu ni mhanga kwa ajili ya Msikiti wa
Al-Aqsa" na "Baki hai Palestina".
Siku ya Jumamosi, jeshi la utawala ghasibu wa Israel
liliwashambulia kwa makombora waumini wa Kipalestina waliokuwa wakisali
Sala ya Alfajiri katika Skuli ya Al-Tabeen katika kitongoji cha
Al-Darj katika mji wa Ghaza, ambapo Wapalestina wasiopungua 100 waliuawa
shahidi na wengine wengi walijeruhiwa.
Wengi wa waliouawa shahidi katika jinai hiyo walikuwa watoto,
wafanyakazi wa serikali, wahadhiri wa vyuo vikuu na shakhsia wa kidini
ambao hawakuhusika kwa namna yoyote na harakati za kisiasa au za
kijeshi.../