Makumi ya watu waripotiwa kuuawa katika shambulizi la Israel mjini Gaza
Makumi ya watu waripotiwa kuuawa katika shambulizi la Israel mjini Gaza

Chanzo cha picha, Reuters
Shirika la ulinzi wa raia linalodhibitiwa na Hamas katika ukanda wa Gaza linasema makumi ya watu wameuawa katika shambulio la anga la Israel dhidi ya makazi katika shule moja mjini Gaza.
Jeshi la Israel lilimethibitisha kushambulia eneo hilo siku ya Jumamosi, na kuelezea lengo la shambulio hilo lilikuwa ni kuharibu kituo mawasiliano cha Hamas kilichowekwa katika shule hiyo.
Kulingana na ajenti wa ulinzi wa raia wa Gaza, shambulio katika wilaya ya Daraj lilisababisha vifo vya takriban watu 90 na kuwajeruhi makumi ya wengine. BBC haijafanikiwa kuthibitisha takwimu hizo.
"Idadi ya waliofariki sasa ni kati ya 90 hadi 100 na kuna makumi ya wengine waliojeruhiwa," msemaji wa shirika hilo Mahmud Bassal aliliambia shirika la habari la AFP.
"Roketi tatu za Israel zilipiga shule iliyokuwa inawahifadhi Wapalestina waliokimbia makazi yao."
Hapo awali katika chapisho la Telegram alielezea tukio hilo kama "mauaji ya kutisha" akisema wafanyakazi walikuwa wakijaribu kudhibiti moto ili kuwaokoa waliojeruhiwa.
Wanajeshi wa Israel walisema "wamewashambulia magaidi wa Hamas wanaoendesha shughuli zao ndani ya kituo cha udhibiti wa Hamas kilichowekwa katika shule ya Al-Taba'een".