Mapigano katika eneo la Kursk yanaingia siku ya tatu, Urusi yasema
Mapigano katika eneo la Kursk yanaingia siku ya tatu, Urusi yasema

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Mapigano makali yanayoendelea katika eneo la Kursk nchini Urusi yameingia siku ya tatu, na juhudi za kuwatimua wanajeshi wa Ukraine nchini humo "zinaendelea", wizara ya ulinzi ya Moscow imesema.
Urusi inasema kuwa takriban wanajeshi 1,000 wa Ukraine, wakiwa na vifaru na magari mengine ya kivita, walivuka mpaka siku ya Jumanne.
Takribani watu 3,000 wamelazimika kuhama eneo hilo, kwani mapigano yanayoendelea ya kijeshi yamesababisha vifo vya watu wanne, naibu Gavana wa Kursk Andrei Belostotsky alisema Alhamisi.
Jeshi la Ukraine limeendelea kusalia kimya kuhusu madai hayo, lakini mshauri mkuu wa Rais Volodymyr Zelensky amelaumu "uchokozi usio na shaka wa Urusi" kwa "hatua zozote za kijeshi".
Mykhailo Podolyak, msaidizi wa muda mrefu wa Rais Zelensky aliongeza: "Vita ni vita, vyenye sheria zake, ambapo mchokozi huvuna matokeo yanayolingana."
Wizara ya ulinzi ya Urusi ilisema maendeleo na "majaribio ya mafanikio" yaliyofanywa na jeshi la Kiukreni katika wilaya za Sudzhansky na Korenevsky huko Kursk yalizuiwa katika juhudi za pamoja kutoka kwa Huduma ya Usalama ya Shirikisho (FSB) na jeshi.
Kremlin ilisema Ukraine imepoteza wanajeshi 660 tangu kuanza kwa mapigano huko Kursk.
Bw Belostotsky alidai kuwa vikosi vya Kyiv vimeanza kurudi nyuma kutoka eneo hilo. BBC haiwezi kuthibitisha idadi ya vifo katika mizozo inayoendelea, na vifo vinavyoripotiwa na wapinzani mara nyingi si uwakilishi wa kweli wa hali hiyo mashinani.