Shambulizi la Israel laua zaidi ya watu 70 Gaza - mkuu wa hospitali
Shambulizi la Israel laua zaidi ya watu 70 Gaza - mkuu wa hospitali

Chanzo cha picha, Reuters
Shambulizi la anga la Israel dhidi ya jengo la shule inayowahifadhi Wapalestina waliofurushwa katika mji wa Gaza limeua zaidi ya watu 70, mkurugenzi wa hospitali moja ameambia BBC.
Fadl Naeem, mkuu wa hospitali ya al-Ahli ambako majeruhi wengi walifikishwa, alisema hao ni waathiriwa ambao wametambuliwa hadi sasa, huku miili mingine ikiwa imeharibiwa vibaya kiasi cha kutoweza kutambuliwa.
Alisema hali ni "janga", na madaktari hawakuweza kuwatibu waliojeruhiwa vibaya.
Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) alisema shule ya al-Taba’een "inatumika kama kituo cha kijeshi cha makundi ya Hamas na Islamic Jihad" na takriban "wanamgambo" 20 wanafanya kazi hapo. Hamas wanakanusha hili.
Makadirio ya awali ya idadi ya waliofariki pia yalikuwa kadhaa, huku huduma ya ambulensi inayoendeshwa na wizara ya afya ya Hamas ikisema zaidi ya 60 wameuawa, kulingana na shirika la habari la AP.
Shirika la ulinzi wa raia lilikadiria idadi hiyo kuwa zaidi ya 90. BBC haijathibisha takwimu kutoka upande wowote.
Israel imeshambulia makazi kadhaa ya aina hiyo huko Gaza katika wiki chache zilizopita.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, majengo 477 kati ya 564 ya shule huko Gaza yalishambuliwa moja kwa moja au kuharibiwa kufikia Julai 6, na angalau 13 yakilengwa tangu wakati huo.