Uhispania: Polisi wanamsaka kiongozi wa zamani Catalonia aliyerejea kutoka uhamishoni
Uhispania: Polisi wanamsaka kiongozi wa zamani Catalonia aliyerejea kutoka uhamishoni

Chanzo cha picha, Reuters
Polisi mjini Barcelona wanamsaka kiongozi wa zamani wa Catalonia anayepigania kujitenga kwa eneo hilo, Carles Puigdemont, ambaye alirejea nchini Uhispania baada ya kukaa uhamishoni kwa miaka saba licha ya kukabiliwa na hati ya kukamatwa.
Polisi wa Mossos d'Esquadra - wameweka vizuizi vya barabarani ndani ya Barcelona na kuelekea nje ya jiji kama sehemu ya Operesheni Jaula - au "ngome" - inayolenga kumpata Bw Puigdemont, ambaye alionekana akitoka kwenye mkutano asubuhi ya leo.
Kwa muda mrefu wa miaka kadhaa iliyopita ameishi Brussels, baada ya polisi kumfungulia mashtaka yanayohusishwa na kushindwa kwa jitihada za kupata uhuru wa Catalonia mwaka wa 2017.
Wakati huo, viongozi wanaounga mkono uhuru wa Catalonia akiwemo Bw Puigdemont walipanga kura ya maoni - ambayo iliamuliwa na mahakama ya kikatiba ya Uhispania kuwa haramu- na baadaye kutangaza uhuru wa eneo hilo.
Madrid iliweka sheria ya moja kwa moja kwenye eneo hilo muda mfupi baadaye na Bw Puigdemont akakimbilia Ubelgiji.
Siku ya Alhamisi asubuhi, Bw Puigdemont alihutubia kwa ufupi mamia ya wafuasi waliokusanyika karibu na bunge la Catalonia mjini Barcelona, muda mfupi kabla ya kuteuliwa kwa mkuu mpya wa serikali ya Catalonia.
Alisema amerejea "kuwakumbusha kwamba bado tuko hapa" na kuongeza: "Kupiga kura ya maoni si kosa na kamwe haitakuwa kosa." Bw Puigdemont kisha akatoweka.