Uingereza yaitaka Iran kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israeli
Uingereza yaitaka Iran kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israeli

Chanzo cha picha, 10 Downing Street
Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer ameitaka Iran "kujizuia" kuishambulia Israeli wakati wa mazungumzo ya simu na rais mpya wa Iran.
Sir Keir alimwambia Masoud Pezeshkian kulikuwa na "hatari kubwa ya kufanya makosa na sasa ulikuwa wakati wa kutulia na kuzingatia kwa makini".
Ni mazungumzo ya kwanza kati ya waziri mkuu wa Uingereza na rais wa Iran tangu Machi 2021 wakati kiongozi wa zamani wa Uingereza Boris Johnson alipozungumza na Hassan Rouhani.
Mazungumzo yao ya dakika 30 yanafanyika wakati Uingereza ikitoa taarifa ya pamoja na Marekani, Ufaransa, Italia na Ujerumani - kuitaka Iran kukomesha vitisho vyake vya kuishambulia Israeli.
Waliitaka Iran "kuacha vitisho vyake vinavyoendelea vya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Israeli na kujadili madhara makubwa kwa usalama wa kikanda iwapo shambulio kama hilo litatokea".
Viongozi hao pia walizungumzia suala la kuunga mkono "ulinzi wa Israeli dhidi ya uvamizi wa Iran na mashambulizi ya makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Iran".
Hofu ya kutokea kwa mzozo mkubwa huko Mashariki ya Kati imekuwa ikiongezeka kufuatia mauaji ya hivi karibuni ya viongozi wakuu wa Hezbollah na Hamas.
Siku ya Jumapili, Marekani ilithibitisha kuwa imetuma nyambizi inayoongozwa na kombora katika eneo hilo kujiandaa kutokana na wasiwasi huu.
Nyambizi hiyo inaweza kubeba hadi makombora 154 ya Tomahawk, ambayo hutumiwa kulenga nchi kavu.