Ukraine yadai kudhibiti kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi
Ukraine yadai kudhibiti kilomita za mraba 1,000 za eneo la Urusi

Chanzo cha picha, Reuters
Kamanda mkuu wa Ukraine amesema vikosi vya Kyiv vinadhibiti kilomita za mraba 1,000 za ardhi ya Urusi huku wakiendeleza uvamizi wao mkubwa wa kuvuka mpaka katika miaka miwili na nusu ya vita.
Kamanda Oleksandr Syrskyi alisema Ukraine iliendelea "kuendesha operesheni ya kimkakati katika eneo la Kursk" siku saba baada ya kuanza.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alisema Urusi imeleta vita kwa wengine na sasa vinarejea kwao.
Lakini kiongozi wa Urusi Vladimir Putin alielezea shambulio hilo kama "uchokozi mkubwa" na akaamuru vikosi vya Urusi "kumfukuza adui nje ya eneo letu".
Idadi inayoongezeka ya watu wamehamishwa kutoka eneo la magharibi mwa Urusi kwa usalama wao, huku wengine 59,000 wakiamriwa kuondoka.
Gavana wa eneo hilo alisema baadhi ya vijiji 28 vimetekwa na vikosi vya Ukraine, na kwamba raia 12 wameuawa na "hali bado ni ngumu".
Wanajeshi wa Ukraine walifanya shambulizi lao la kushtukiza Jumanne iliyopita, na kusonga hadi maili 18 (km 30) kuingia Urusi.
Mashambulizi hayo yanasemekana kuongeza ari kwa upande wa Ukraine, lakini wachambuzi wanasema mkakati huo unaleta hatari mpya kwa Ukraine.
Chanzo kikuu cha kijeshi cha Uingereza, ambacho hakikutaka jina lake litajwe, kiliiambia BBC kwamba kuna hatari Moscow itaghadhabishwa na uvamizi huo kiasi kwamba inaweza kuongeza mashambulizi yake yenyewe dhidi ya raia na miundombinu ya Ukraine.