Ukraine yaendelea na mashambulizi yake dhidi ya Urusi
Ukraine yaendelea na mashambulizi yake dhidi ya Urusi

Chanzo cha picha, IZ.RU/Reuters
Wanajeshi wa Ukraine wanaendelea na mashambulizi yao katika eneo la Kursk magharibi mwa Urusi, huku mashambulizi yao ya kushtukiza ya kuvuka mpaka yakiingia siku ya tano.
Urusi imetangaza operesheni ya "kukabiliana na ugaidi" katika maeneo matatu, huku ikijitahidi kukabiliana na uvamizi huo.
Siku ya Ijumaa Wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema kuwa "inaendelea kuwakabili" wanajeshi wa Ukraine, ambao ilidai kuwa wamepoteza zaidi ya wanajeshi 280 katika muda wa saa 24 zilizopita - idadi ambayo haijathibitishwa kikamilifu.
Ripoti zinaonyesha kuwa wanajeshi wa Ukraine wanafanya kazi zaidi ya kilomita 10 ndani ya Urusi - hatua kubwa zaidi ya Kyiv tangu Moscow ilipoanzisha uvamizi wake kamili wa Ukraine mnamo Februari 2022.
Ukraine haijakiri hadharani uvamizi huo, lakini Rais Volodymyr Zelensky alisema wiki hii kwamba Moscow lazima "ihisi" matokeo ya uvamizi wake.