Wadukuzi wa Korea Kaskazini wanajaribu kuiba siri za nyuklia na kijeshi, Marekani, Uingereza zasema
Wadukuzi wa Korea Kaskazini wanajaribu kuiba siri za nyuklia na kijeshi, Marekani, Uingereza zasema

Chanzo cha picha, Getty Images
Wadukuzi wa Korea Kaskazini wanajaribu kuiba siri za nyuklia na kijeshi kutoka kwa serikali na makampuni binafsi duniani kote, Uingereza, Marekani na Korea Kusini zimeonya.
Wanasema kundi hilo, linalojulikana kwa majina Andariel, Onyx Sleet na DarkSeoul, miongoni mwa mengine linalenga vyombo vya ulinzi, anga, nyuklia na uhandisi ili kupata taarifa za siri, kwa lengo la kuendeleza mipango na malengo ya kijeshi na nyuklia ya Pyongyang.
Kundi hilo limekuwa likitafuta habari katika sekta mbalimbali, kuanzia urutubishaji wa urani hadi mizinga, nyambizi na torpedo na limelenga Uingereza, Marekani, Korea Kusini, Japan, India na nchi nyingine, kwa mujibu wa mwandishi wa usalama wa BBC Gordon Corera.
Iinashukiwa kushambulia vituo vya anga vya Marekani, NASA na makampuni ya ulinzi.
Onyo la hali ya juu kuhusu kundi hili linaonekana kuwa ishara kwamba shughuli yao, ambayo inachanganya ujasusi na faida, inatia wasiwasi mamlaka kwa sababu ya athari zake kwa teknolojia nyeti na maisha ya kila siku.
Marekani inasema kundi hilo linafadhili shughuli zake za ujasusi kupitia operesheni dhidi ya taasisi za afya nchini humo.