Wanajeshi wa Ukraine wapo kilomita 30 ndani ya eneo la Urusi
Wanajeshi wa Ukraine wapo kilomita 30 ndani ya eneo la Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanajeshi wa Ukraine wamesonga mbele hadi kilomita 30 ndani ya Urusi, katika hali ambayo imekuwa uvamizi mkubwa na muhimu zaidi tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake dhidi ya Ukraine mnamo Februari 2022.
Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa vikosi vyake vimewakabili wanajeshi wa Ukraine karibu na vijiji vya Tolpino na Obshchy Kolodez, huku mashambulizi katika eneo la Kursk yakiingia siku ya sita.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje Maria Zakharova alishutumu Ukraine kwa "kuwatisha watu wenye amani wa Urusi".
Rais Volodymyr Zelensky, ambaye alikiri moja kwa moja shambulio hilo kwa mara ya kwanza katika hotuba jana usiku, alisema mashambulizi 2,000 ya kuvuka mpaka yameanzishwa na Urusi kutoka Kursk majira haya ya joto.
"Silaha, makombora, ndege zisizo na rubani. Pia tumerekodi mashambulio ya makombora, na kila shambulio kama hilo linastahili jibu sahihi," Bw Zelensky aliiambia nchi katika hotuba yake ya usiku kutoka Kyiv.
Afisa mmoja mkuu wa Ukraine aliliambia shirika la habari la AFP kwamba maelfu ya wanajeshi walishiriki katika operesheni hiyo, ikiwa ni zaidi ya uvamizi mdogo ulioripotiwa hapo awali na walinzi wa mpaka wa Urusi.
Wakati vikundi vinavyoungwa mkono na Ukraine vimeanzisha mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvuka mpaka, mashambulizi ya Kursk yanaashiria shambulio kubwa lililoratibiwa katika eneo la Urusi na vikosi vya kawaida vya Kyiv.