Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania wakamatwa
Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania wakamatwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Wanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu na Freeman Mbowe wanashikiliwa na Jeshi la Polisi tangu usiku wa kuamkia leo kwa kile walichodaiwa kuhusika kuandaa maandamano ya vijana kwenye maadhimisho ya Siku ya vijana duniani hii leo.
Kadhalika, Jeshi hilo lilidaiwa kuwashikilia na kisha kuwaachia kwa kuwalazimisha vijana wa chama hicho kurejea mikoa wanayotokea ili wasishiriki maadhimisho hayo waliyoyapanga mkoani Mbeya, kusini mwa Tanzania.
Msemaji wa chama hicho cha upinzani, John Mrema ameiambia BBC kuwa hadi asubuhi ya leo hawajui ni kituo gani cha polisi ambapo viongozi hao watatu wanashikiliwa.
“Hatufahamu wanashikiliwa wapi ila wapo mikononi mwa polisi, tunafuatilia sambamba na mawakili wetu… Tutatoa taarifa zaidi baadaye mchana,” alisema.
Pia alisema makundi makubwa ya vijana waliokuwa kwenye mabasi ya kukodi yalisimamishwa na kukamatwa walipokuwa wakisafiri kwenda Mbeya kwa ajili ya sherehe hizo.
Mrema alisema hadi kufikia asubuhi ya leo polisi hawajaruhusu vijana hao kufika Mbeya na badala yake wamewalazimisha vijana hao kurejea katika mikoa yao wakiwa chini ya ulinzi.
Siku ya jana, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa kuwa vijana hao wa Chadema walipanga maandamano ambayo yalikuwa yana viashiria vya kuvunja amani.
Katika taarifa iliyotolewa na jeshi hilo ilisema kuwa kiongozi mmoja wa vijana wa chama hicho alikuwa akihimiza kuwepo maandamano kama yale yaliyofanyika nchini Kenya yaliyohusisha vijana maarufu Gen Z.
Jitihada za kupata jeshi la polisi bado zinaendelea kuhusiana na taarifa hii.
Katika hatua nyingine, Jeshi la polisi nchini Tanzania limesema kuwa halijapiga marufuku kufanyika kwa mikutano ya nje ya hadhara na ile ya ndani, ili mradi inafuata matakwa ya sheria ya nchi.
Polisi imefafanua kuwa kilichopigwa marufuku ni mkusanyiko uliokuwa umeitishwa na viongozi wa Chadema huko jijini Mbeya kwa kivuli cha kuadhimisha Siku ya Vijana Duniani. Taarifa imeeleza.