Je hiki ndicho kilichomponza Gachagua?
Je hiki ndicho kilichomponza Gachagua?
Mahakama Kuu nchini Kenya imeamua kuwa Kithure Kindiki anaweza kuapishwa kuwa Naibu Rais Mpya baada ya kutupilia mbali ombi la Naibu wa Rais aliyeondolewa madarakani Rigathi Gachagua.
Wakati likitoa uamuzi huo, jopo la majaji watatu lilisema kuwa afisi ya kikatiba ya naibu rais haiwezi kuachwa wazi.
Mgombea mwenza wa Rais William Ruto katika uchaguzi uliopita Rigathi Gachagua alitimuliwa na bunge la Kenya mapema mwezi huu. Baadaye, Rais Ruto alimteua Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki kama Naibu Rais mpya na Bunge la kitaifa likapiga kura kuunga mkono uteuzi wake.
Imeelezwa kwamba Naibu Rais wa Kenya Rigathi Gachagua ameng’olewa madarakani kwasababu ya kuhujumu idara ya ujasusi na mahakama, kukiuka kiapo chake na Katiba na kuchochea siasa za ukabila.
Lakini inawezekana hata bila kukusudia, Gachagua mwenyewe ameeleza umma vyema kiini cha kung’olewa kwake madarakani, pegine vyema zaidi kuliko wachambuzi wa kisiasa wanavyozungumzia.
“Mimi ndio mtu pekee katika baraza la mawaziri na serikali ninayeweza kusimama na kumwambia William Ruto ukweli kwamba ‘bwana wee, hii sio sawa, hili swala la Adani sio zuri kwa nchi, kuna rushwa kubwa sana, hili swala la nyumba za makazi linalazimishwa kwa Wakenya na hawalipendi, usililazimishie tafadhari’” alisema Gachagua baada ya kutoka hospitali akiwa na sura iliyokosa nuru, sauti ya upole na akiwa makini katika kuchagua maneno ya kuzungumza.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema hata kama siasa za Kenya zawezakuwa tofauti na kwingineko Afrika Mashariki na hata Afrika kwa ujumla, lakini miiko ya u-Makamu au uNaibu Rais - hata kama haijaandikwa mahala na muhusika hasomewi aingiapo kazini hubaki kuwa ile ile - iwe Kenya, Tanzania, Marekani au kwingineko.
“Mimi mara yangu ya kwanza kabisa kujua kuna tatizo ni baada ya Rigathi Gachagua kuanza kuweka picha mitandaoni akiwa anaingia kazini saa kumi na mbili asubuhi” anasema Ezekiel Kamwaga, mwandishi wa habari na mchambuzi wa siasa za Afrika.
Kwa kutuma picha zinazoweza kutafsiriwa kuwa Gachagua ni mchapa kazi kuliko bosi wake, Naibu huyo wa Rais alikiuka kanuni mojawapo ambayo Kamwaga anaiita kutokutaka kung’ara kuliko bosi wake. Lakini kwa kuendelea kudai kuwa yeye Gachagua ana ubi ana Rais, Gachagua alikiuka kanuni nyigine ya msingi kwamba urais hauna ubia.
Kamwaga anaongeza pia kwamba sifa kubwa ya aidha Naibu au Makamu wa Rais ni mtu anayeweza kuwa na ‘low profile’ (asiyeonekana), anayefanya mambo yake kichinichini. Anaongeza kuwa Naibu Rais hawezikuwa mtu anayeng’ara aidha sawa au kumzidi rais.
“Hili ndio jambo ambalo lilitokea Marekani juzi. Huyu Kamala Harris (Mgombea Urais), watu wengi waliamini kwamba mtu ambaye angeweza kumpa kura nyingi zaidi ni yule Josh Shapiro. Alikuwa ana sifa nyingi sana za kumfaa, lakini watu wakamwambia ‘Kamala, Shapiro atakufunika, tafuta mtu mwingine.’ Ndo kumpata huyu mtu (Tim Walz) ambaye hata hajulikani” anasema Kamwaga.
Hoja ya Kamwaga inaungwa mkono na Profesa William A Galtson aliyeandika katika uchambuzi wake katika wavuti ya taasisi bobezi ya utafiti na fikra tunduizi Brookings Institute hapo Agosti 2024 akidadisi sababu za Harris kumuacha Shapiro anayetoka Pennsylvania, moja ya jimbo linaloshikilia matokeo ya urais wa Marekani.
“Inasemekana Harris alitaka mtu anayeweza kuwa mtiifu, atakayemuunga mkono nyakati zote, na inawezekaa alimuona (Tim) Walz kuwa na uwezekano mdogo wa kugawanyika kati ya huduma kwa utawala wake (Harris) na tamaa za kibinafsi za kisiasa,” anaandika Prof Gatson.
Wadadisi waataja baadhi ya sifa na hulka bora za Makamu au Naibu Rais ni pamoja na kutokuwa mwerevu kuliko rais na ukubali kuwa kiti cha nyuma. Umsaidie Rais kuongeza kura lakini ujue kuwa Urais hauna ubia. Aidha usiwe na matamanio ya kuwa rais au usiyaonyeshe wazi wazi, tena mwanzoni tu mwa muhula wenu madarakani. Lingine la muhimu ni kwamba Makamu/Naibu anapaswa kuridhika kumfanya rais wake ang’are.
Ndani ya miaka miwili hii iliyopita, Gachagua ameonesha hulka inayokiuka miiko mingi ya u-Naibu. Inawezekana mazingira ya wakati ule wa uchaguzi yalimfanya Ruto kumchagua Gachagua akifikiria tu kura za Mlima Kenya ambazo atazileta akasahau hulka zingine za Gachagua, lakini baada ya kuingia Ikulu, Gachagua alipaswa kuzivaa hizi sifa zingine mapema iwezekanavyo aepuke haya yaliyomkuta.
Historia ya mahusiano ya Rais na makamu wake Kenya
Ikumbukwe kwamba tangu kupatikana kwa Uhuru wake Desemba 12 1962 Kenya imekuwa na makamu/Manaibu Rais 12 ambao wamewahudumia Marais watano. Uhusiano kati yao na wakubwa wao ulikuwa tofauti mno, huku ndoa ya kwanza kuvunjika ikiwa ile ya muanzilishi wa taifa Jommo Kenyatta na makamu wake wa kwanza Jaramogi Oginga Odinga. Wawili hao walifanya kazi pamoja kwa mwaka mmoja pekee kabla ya Oginga Odinga kuondoka madarakani na kuanza maisha ya kibaridi cha upinzani 14 Aprili 1964. Malumbano yao aliyanakili kwenye kitabu chake kilichochapishwa 1966 chenye jina ‘No longer Uhuru.’
Aliyepokezwa majukumu hayo Joseph Murumbi, naye alihudumu kwa siku 120 pekee kabla ya kujiuzulu. Wanahistoria wanasema kwamba aliamua kuondoka kwa kuhofia maisha yake, kwani hakukubaliana na hatua ambazo serikali aliyoihudumia ilikuwa inachukuwa hasa kuhusu suala la mashamba.
Daniel Moi alihudumu kwa zaidi ya miaka 10 kama Makamu wa Kenyatta na laifanya nae kazi vyema bila kuonekana hadharani au kwa siri kuwa alikuwa anatofautiana na bosi wake na hatimaye akachukua mamlaka ya uongozi mwaka 1978 Kenyatta alipofariki. Hatahivyo, kulikuwa na njama za baadhi ya wabunge na viongozi serikalini kujaribu kubadili katiba kumzuia kurithi kiti hicho lakini mipango hiyo ilitibuliwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa wakati huo Charles Njonjo wakati.
Moi alihudumu na Mkamu wanne,mmoja wao akiwa ni Josephat Karanja ambaye mnamo mwaka 1989 alipokumbwa na ‘kura ya kutokuwa na imani naye’ bungeni mnamo kwa madai ya kula njama za kumpindua Moi. Tofauti na Gachagua, Karanja alijiuzulu.
George Saitoti alipokezwa mamlaka hayo na kuhudumu kwa miaka 13, ila kwa awamu mbili …alijipata kwenye kibaridi wakati wa kwanza Januari 1998 alipopokea taarifa kwamba ameondolewa kama makamu wa Rais. Kwa muda wa mwaka mmoja baada ya hapo, Moi alihudumu bila makamu, wakati huo madai ya wawili hao kutoaminiana yakitajwa.
Saitoti alirejeshwa kazini 1999 hadi 2002 alipoondoka tena na Musalia Mudavadi kupokezwa mamlaka kwa miezi miwili tu, kabla ya uchaguzi mkuu ulioashiria mwisho wa miaka 24 ya uongozi wa Moi.
William Ruto ndiye Naibu wa Rais wa kwanza chini ya katiba mpya iliyoasisiwa 2010, na japo waliingia madarakani wakijinadi kama ndugu na hata kuvalia sawa, usuhuba wake na Uhuru Kenyatta ulingia dowa na ukawa mchungu walipoanza awamu yao ya pili 2017. Japo walizozana ndani kwa ndani, Ruto hakutamka wala kumkosea heshima Rais wake hadharani, hadi mwaka mmoja kabla ya kura ya 2022 alipomuoomba Uhuru kutuwadhuru Watoto wake na kusema kwamba yeye sio mlevi, ishara kwamba alikuwa anamsuta mkubwa wake.
Mahusiano ya Marais na Makamu wao Afrika Mashariki
Hadi sasa, Tanzania imewahi kuwa na Makamu wa Rais kumi. Baadhi yao walikuwa ni watu wenye elimu na ujuzi wa kipekee na wa hali ya juu sana, lakini mienendo na hulka zao inatoa tafsiri kwamba walizifahamu nafasi zao na matarajio juu yao vizuri sana.
Wengi watamkumbuka Dr. Mohamed Gharib Bilal, mbobezi wa fizikia ya nyuklia. Lakini alitulia katika nafasi yake ya Umakamu akiridhika kuzunguka huku na kule kukata utepe wa uzinduzi wa miradi na majengo hata pakaibuka utani kwamba alitembea na mkasi mfukoni wakati wote tayari.
Inaweza kupita hata wiki kadhaa hujamuona Makamu wa Rais Dr Philp Mpango - mchumi mbobezi aliyepikwa na shirika la fedha la kimataifa (IMF) na chuo kikuu cha Harvard – kwenye kurasa za mbele za magazeti.
Lakini hata anapotokea, huwezi kumsikia akichokonoa sera za uchumi za Rais Samia Suluhu Hassan. Hotuba yake ya tarehe 21 Oktoba akifungua mkutano wa kusherehekea miaka 30 ya Taasisi ya Utafiti wa uchumi na Jamii (ESRF) alilia na vijana wenye tabia ya kupenda ‘Mishangazi’ ili kujipatia kipato kirahisi.
Siku chache zilizopita, mwanahabari nguli wa Uganda Charles Onyango Obbo alitukumbusha juu ya Edward Ssekandi, kama moja ya Makamu wa Rais wa Uganda aliyedumu zaidi madarakani – hakuwa Makamu aliyetafuta kupimana ubavu na ‘bosi’ wake.
“Kinachomtofautisha Ssekandi ni kwamba huenda alikuwa Makamu wa Rais pekee barani Afrika ambaye hakuwahi hata mara moja kuingia katika matatizo na bosi wake Rais Yoweri Museveni, au mtu mwingine yeyote. Ingepita hata zaidi ya nusu mwaka bila kuonekana kwenye vyombo vya habari, na mara chache tu picha zingeibuka kwenye mitandao ya kijamii za yeye akinywa au kucheza mziki peke yake,” anaandika Obbo.
Hiki kilimshinda Gachagua. Aliamini yeye na bosi wake wako sawa na wana ubia katika urais. Mara nyingi alikumbusha jinsi alivyoleta kura za anakotokea Mlima Kenya, na kwamba kama alivyo Ruto, yeye pia alipigiwa kura na wananchi.
Obbo anamalizia kwa kutoa somo la utumishi wa Ssekandi kwamba Afrika hii, hii siri ya kustawi na kudumu katika nafasi ya uNaibu ni kufanya kila uwezalo usiwe Naibu, na kumudu uwezo wa kutoonekana.
Gachagua ataendelea kuamini ameonewa na kuchezewa rafu na boss akiamini alikuwa anaenenda kwa mujibu wa Katiba. Lakini isivyo bahati kwake, alipumbazwa na kilichoandikwa kweye Katiba pekee akasahau miiko isiyoandikwa wala kufundishika darasani.