Hospitali katika Gaza ni "uwanja wa vita," na watu waliohamishwa wanajiuliza: Tunaenda wapi?
Mkuu wa shirika la afya Ulimwenguni (WHO), ametoa wito wa kukomeshwa kwa "mashambulizi katika hospitali" huko Gaza.
Bwana Tedros Adhanom alisema kuwa hospitali za Gaza kwa mara nyingine tena zimekuwa "uwanja wa vita" na kwamba mfumo wa afya uko chini ya "tishio kubwa."
Madai ya Adhanom yanakuja baada ya kushambuliwa na kuhamishwa kwa Hospitali ya Kamal Adwan na jeshi la Israel Ijumaa iliyopita, ambacho ni kituo kikubwa cha mwisho cha afya kinachofanya kazi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, licha ya mashambulizi katika hospitali mbili katika mji wa Gaza siku ya Jumapili.
Jeshi la Israel linasema kuwa maeneo mawili kati ya haya yanatumiwa na Hamas kama "vituo vya kutoa amri," jambo ambalo vuguvugu hilo limekanusha mara kwa mara.
Mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni alitoa wito huo baada ya mashirika ya kutetea haki za binadamu pia kupaza sauti zao, wakitaka kuachiliwa mara moja kwa mkurugenzi wa Hospitali ya Kamal Adwan, Dk Hossam Abu Safiya, ambaye alikamatwa na vikosi vya Israeli wakati wa mashambulizi dhidi ya hospitali hiyo.