Idadi ya watoto wanaofariki kwa baridi kali Gaza yafikia sita
Binti Sila alikuwa na umri wa chini ya wiki tatu wakati mama yake Nariman alipogundua kuwa hatikisiki tena.
"Niliamka asubuhi na kumwambia mume wangu kuwa mtoto alikuwa hajatikisika kwa muda. Alifunua uso wake na kumkuta amekuwa wa bluu, ametafuna ulimi, huku damu zikimtoka mdomoni," anasema Nariman al-Najmeh.
Katika hema lao lililo ufukweni kusini mwa Gaza, Nariman anaishi na mumewe, Mahmoud Fasih, na watoto wao wawili wadogo - Rayan, mwenye umri wa miaka minne, na Nihad, mwenye umri wa miaka miwili na nusu.
Kifo cha Sila kinafanya idadi ya watoto waliofariki kutokana na baridi kali Gaza kufikia sita ndani ya kipindi cha wiki mbili kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo.
Mama yake Sila, Nariman anasema mwanawe alizaliwa katika hospitali moja katika eneo la Khan Younis akiwa na afya nzuri.
"Afya yake ilikuwa nzuri, namshukuru Mungu, lakini ghafla, alianza kuathiriwa na baridi," anasema Nariman. "Niliona akipiga chafya na alionekana kuumwa, lakini sikutarajia angekufa kwa sababu hiyo."
Sila alilazwa siku ya Jumatano iliyopita katika hospitali ya Nasser huko Khan Younis, ambapo Dk Ahmad al-Farra, mkurugenzi wa idara ya watoto, alisema alikuwa na "baridi kali, na kusababisha viungo muhimu kuacha kufanya kazi na kupelekea, mshtuko wa moyo, na hatimaye kifo."
Nyakati za usiku joto hupungua hadi nyuzi joto 7C huko Gaza, huku kukiwa na “vikwazo vya Israel katika kupeleka chakula na misaada mingine,” kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, na hivyo kuzidisha mzozo wa kibinaadamu katika eneo hilo.
Lakini Israel inakanusha kuwa inazuia misaada.