Iran yathibitisha kumkamata mwandishi wa habari wa Italia
Serikali ya Iran imethibitisha kwa mara ya kwanza kwamba mwanahabari wa Italia, Cecilia Sala alikamatwa nchini humo kwa misingi ya "kukiuka sheria za nchi hiyo.”
Haya yanajiri baada ya msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuliambia gazeti la kila siku la Italia, La Repubblica kwamba kesi ya Bi Sala inaweza kuingiliana na kukamatwa kwa raia wa Iran, mjini Milan hivi karibuni kwa ombi la Marekani.
Sala, mwandishi wa habari mwenye umri wa miaka 29 na mtangazaji wa podikasti maarufu ya habari, alizuiliwa nchini Iran tarehe 19 Disemba, siku moja kabla ya kurudi nyumbani kutoka katika safari ya kuripoti. Anaripotiwa kuzuiliwa katika gereza la Tehran la Evin.
Tarehe 16 Disemba, raia wa Iran, Mohammad Abedini alikamatwa mjini Milan, Italy kwa tuhuma za kupeleka vifaa vya kielektroniki vya ndege zisizo na rubani kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), na kusababisha vifo vya wanajeshi watatu wa Marekani.
Kwa sasa Marekani inataka Bw Abedini apelekwe Marekani.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani aliyenukuliwa na La Repubblica alisema Sala amekamatwa kama mtaji wa kisiasa.
Si serikali ya Italia wala ya Iran ambayo imethibitisha uhusiano wowote kati ya Cecilia Sala na Mohammad Abedini.
Hata hivyo, tarehe 21 Desemba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilimwita mwanadiplomasia mkuu wa Italia kuhusu kukamatwa kwa Abedini.
Italia inasema kukamatwa kwa Sala ni jambo lisilokubalika na Waziri wa Mambo ya Nje, Antonio Tajani amesema juhudi za kutaka aachiliwe bado ni ngumu.